Header Ads Widget

CCM KATA YA MAGOMENI WAPONGEZA MKOA KUSIMAMISHA UCHAGUZI WA MWENYEKITI WA WAZAZI


Na Mwandishi Wetu

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Magomeni, Wilaya ya Kinondoni, wamepongeza uongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusitisha uchaguzi wa kuziba nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa kata hiyo uliokuwa ufanyike Septemba 24, 2026.

Wanachama hao kutoka matawi tofauti wamesema uamuzi huo umetenda haki na kulinda misingi ya chama baada ya kudaiwa kufanyika figisu ya kukatwa jina la mmoja wa wagombea halali.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi Kata, Tatu Ally Khatibu, ameipongeza CCM Mkoa kwa kusikiliza rufaa ya wanachama. "Tunashukuru kwa kukubaliwa kwa rufaa yetu. Sisi ndio wanachama na wenye chama, tumechoka kuburuzwa na kuletewa mtu ambaye hatumfai," amesema.




Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kata ya Magomeni, Mwantumu Baila, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na uongozi wa mkoa kwa uamuzi huo ili kila mtu apate haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Mjumbe mwenzake wa Halmashauri Kuu, Omary Mwaita Omary, amesema uongozi wa wilaya umebagua kwa kukata wagombea bila haki na ameitaka mkoa kuwarudisha wagombea wote wapigiwe kura mezani.

Naye Fatma Omary Kibwana ameomba wagombea wote wanne waliojitokeza waruhusiwe kupigiwa kura ya wazi. "Hatuitaji makundi. Wote tunawafahamu, tutetee uhai wa chama chetu, chama kwanza mtu baadaye," amesema.

Mwenyekiti wa Wazazi Tawi la Makuti A, Joram Makasi na Katibu wake Grace Makero pamoja na Mjumbe wa Shina Namba 5 Sunna, Haji Shaban Sika, wamedai bado kuna makundi yanayoongozwa na viongozi wakubwa yanayowapangia wanachama viongozi na kumuomba mkoa kuyavunja ili demokrasia itawale.

Kwa sasa CCM kipo katika kufanya chaguzi za kuziba nafasi wazi kulingana na sababu mbalimbali, kama vile vifo vya viongozi au kujiuzulu, ambapo michakato ya kuchukua fomu na uteuzi na kupigiwa kura huendeshwa katika ngazi husika.

Miongoni mwa taratibu za CCM kusimamisha au kufuta michakato ya uchaguzi wa ndani pale panapojitokeza ukiukwaji wa taratibu imekuwa ikipokelewa kwa pongezi kubwa na wanachama wanaounga mkono uadilifu. Mara nyingi, maamuzi haya huchukuliwa ili kulinda katiba ya chama, kuzuia mipasuko, na kukabiliana na vitendo vya rushwa au upendeleo.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI