Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema hali ya El Niño nchini inaendelea kuimarika, huku kilele cha hali hiyo kikitarajiwa kufikiwa katika kipindi cha Novemba na Desemba 2026.
Ofisa Habari wa TMA, Ramadhan Omary, amesema El Niño tayari imejijenga na inaendelea kuimarika, hali ambayo imeelezwa kuwa inaweza kuongeza uwezekano wa mvua kubwa katika kipindi cha msimu wa masika.
“Uwezekano wa kuwepo El Niño ni asilimia 100, kwa maana tayari imeshajitengeneza. Kinaendelea kwa sasa ni kuimarika kwa hali hiyo,” amesema Omary.
Kwa mujibu wa Omary, mvua zimeanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo kabla ya msimu wa mvua kuanza rasmi, huku maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria yakitarajiwa kupata mvua kuanzia mwishoni mwa Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba.
Amesema mikoa ya Kagera na Mara ni miongoni mwa maeneo ambayo tayari yameanza kupata mvua za hapa na pale, sambamba na kuwepo kwa ngurumo.
“Zipo ripoti katika mfumo kwamba kuna mvua za hapa na pale, pia kuna ngurumo, hususan katika maeneo ambayo yanazunguka Ziwa Victoria, kwa maana ya mikoa ya Kagera pamoja na Mara,” amesema.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kuimarika kwa El Niño kunaweza kuambatana na ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo, hivyo wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kutoka TMA.






0 Comments