Na Matukio daima App Kilosa Morogoro
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki, kupitia Ofisi ya Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kilosa, imekabidhi madawati 50 yenye thamani ya Sh milioni 12 kwa Shule ya Msingi Mazinyungu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo kurejesha kwa jamii.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwa niaba ya Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, SACC Nethew Ntilicha, Mhifadhi Misitu wa TFS Wilaya za Kinondoni na Ubungo Dotto Ndumbikwa amesema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa TFS kurudisha kwa jamii huku akiwataka wakazi wa Kilosa kuendelea kutunza misitu kwa kuwa faida zinazotokana na uhifadhi wake ndizo zinazowezesha shughuli za kijamii kama utoaji wa msaada huo.
Ndumbikwa amesema TFS inaendelea kushirikiana na wadau katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu, huku akisisitiza kuwa jamii ina nafasi kubwa katika kuhakikisha misitu inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, ameishukuru TFS kwa msaada huo akisema umefika wakati muafaka kutokana na ongezeko la idadi ya watoto wanaojiunga na shule.
Amesema serikali haiwezi kufanya kila kitu bila ushirikiano wa wadau, hivyo akaitaka TFS kuendelea kuifikia shule nyingine zenye mahitaji pia amesisitiza umuhimu wa jamii kupanda na kutunza miti, akisema Kilosa haitakiwi kuwa jangwa, huku akibainisha kuwa walimu wana nafasi muhimu kuwafundisha watoto umuhimu wa uhifadhi ili ujumbe huo usambae katika jamii.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi Kaka Mkuu wa shule hiyo, Marco Ng’ondya, mwanafunzi wa Darasa la Sita, ameishukuru TFS kwa msaada huo akisema awali baadhi ya wanafunzi walilazimika kukaa chini, hali iliyowafanya kupata changamoto katika kuandika, kuchafua sare na kushindwa kumfuatilia mwalimu kwa umakini. Aliahidi kuwa wanafunzi wataitumia fursa hiyo kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo, huku akiomba wadau wengine kuendelea kusaidia shule hiyo kukamilisha mahitaji yaliyopo












0 Comments