Header Ads Widget

BAJETI YA MIKOPO KWA WANAFUNZI ELIMU YA JUU NA VYUO VYA KATI YAPAA HADI SH. TRILIONI 1.06, WANUFAIKA KUFIKIA 292,463

 


Na CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

BAJETI ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati imeongezeka kutoka Sh bilioni 916.7 mwaka wa masomo 2025/2026 hadi kufikia Sh trilioni 1.06 mwaka wa masomo 2026/2027, huku idadi ya wanufaika ikitarajiwa kuongezeka kutoka wanafunzi 252,773 hadi 292,463.

Hayo yamebainishwa  na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP. Salum Hamduni, katika kikao kazi cha 15 kati ya Menejimenti ya HESLB na Maafisa Mikopo kutoka taasisi za elimu ya juu na vyuo vya kati nchini, kilichofanyika leo septemba 23, 2026 jijini Mwanza.

CP. Hamduni alisema ongezeko hilo la bajeti linaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuongeza fursa kwa vijana wa Kitanzania ili waweze kupata elimu ya juu na kutimiza ndoto zao za kielimu.

Ameelwza kuwa katika bajeti hiyo ya Sh trilioni 1.06 kwa mwaka wa masomo 2026/2027, wanafunzi wapya 111,342 wanatarajiwa kunufaika, huku idadi ya jumla ya wanufaika ikifikia 292,463.

“Mwaka uliopita 2025/2026 zilitengwa shilingi bilioni 916.7 zilizowezesha kuwasomesha wanafunzi 252,773, na mwaka huu 2026/2027 zimetengwa shilingi trilioni 1.06 kwa ajili ya kuwagharimia wanafunzi 292,463 wakiwemo wanafunzi 111,342 wa mwaka wa kwanza,” alisema CP. Hamduni.

Hamduni amesema kuwa mikopo ya elimu ya juu ina umuhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuongeza fursa za Watanzania kupata elimu ya juu na kujenga mfumo bora na jumuishi wa elimu na mafunzo.

Aidha CP. Hamduni ameitaka HESLB kuendelea kufanya kazi kwa karibu na menejimenti za vyuo pamoja na Maafisa Mikopo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinawafikia wanafunzi walengwa kwa wakati.


“Ni muhimu mkakumbuka kuwa mnao wajibu wa kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Menejimenti za vyuo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinawafikia walengwa" Alisema Hamduni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia ameeleza kuwa uwekezaji huo umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka na kutoa fursa kwa vijana wa Kitanzania ili kufikia kiwango cha juu cha elimu.

Kiwia ameleza kuwa  pamoja na ongezeko la fedha na idadi ya wanufaika, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha taarifa za wanafunzi zinawasilishwa kwa usahihi na kwa wakati ili mwanafunzi anayestahili aweze kupata huduma anayostahili.


Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia aliwataka Maafisa Mikopo kuendelea kutoa elimu kwa wanufaika kuhusu taratibu za kuomba mikopo, masharti ya kunufaika, namna ya kupata huduma pamoja na wajibu wao baada ya kumaliza masomo.

Aidha amewataka wanafunzi kutumia fursa hizo kwa kusoma kwa bidii ili waweze kuhitimu ndani ya muda uliopangwa na hatimaye kutumia elimu wanayoipata katika kuchangia maendeleo ya taifa.

Kikao hicho kimewakutanisha zaidi ya Maafisa Mikopo 200 kutoka taasisi za elimu ya juu na vyuo vya kati nchini pamoja na viongozi wa wanafunzi kutoka TAHLISO na ZAHILFE.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI