Na Matukio Daima Media, Tabora
MKUU wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Thomas Mnyinga, ameungana na viongozi mbalimbali wa mkoa huo kumpokea Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alipotembelea Kitongoji cha Ipembe, Kijiji cha Majojolo, kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF).
Ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Kijiji cha Majojolo na maeneo mengine ya Wilaya ya Sikonge.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati ya kisasa, jengo la wagonjwa wa nje (OPD), kichomea taka za hospitali, shimo maalumu la kutunzia kondo za nyuma baada ya kujifungua (placenta pit) pamoja na nyumba ya watumishi yenye uwezo wa kuhudumia familia mbili.
Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuwapunguzia wananchi changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya, huku ukisaidia kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi watakaopangiwa kuhudumu katika zahanati hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya, pamoja na viongozi wengine, amepongeza juhudi za JMKF kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hususan katika sekta muhimu ya afya.
Wananchi wa eneo hilo pia wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, wakisema kukamilika kwake kutakuwa hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa kina mama, watoto na jamii kwa ujumla.
Shukrani zimetolewa kwa Jakaya Mrisho Kikwete Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya SC Johnson katika kufanikisha miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Sikonge.









0 Comments