IRUWASA yatangaza zawadi ya Sh 500,000 kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa wahalifu
Na Angel Magesa (UoI), Matukio Daima Media, Iringa
WANANCHI wa Gangilonga, Manispaa ya Iringa, wameingiwa na hofu kufuatia kuongezeka kwa matukio ya wizi wa mita za maji katika nyumba na maeneo ya biashara.
Matukio hayo yanadaiwa kutokea mara kwa mara katika siku za hivi karibuni, hali inayosababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma ya maji inayopimwa, uharibifu wa mali na upotevu wa maji.
Wakazi na wafanyabiashara waliozungumza na Matukio Daima Media wameiomba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuchunguza chanzo cha wizi huo na kubaini mahali mita zinakopelekwa baada ya kuibwa.
Mkazi wa Gangilonga, John Kalinga, alisema wizi huo umeendelea kwa muda na sasa umeanza kuleta hofu kutokana na matukio kujirudia katika maeneo mbalimbali ya mtaa huo.
“Mtaa mzima kila mmoja analalamika kuibiwa mita ya maji. Leo zimeibiwa mita mbili, jana moja na maeneo mengine zimeibiwa mita tatu. Tunaomba idara ya maji ifuatilie tatizo hili,” alisema Kalinga.
Alisema kuna haja ya kuwafuatilia pia watu wanaonunua mita hizo, pamoja na kuweka utaratibu utakaosaidia kulinda mita zilizofungwa nje ya nyumba na maeneo ya biashara.
Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika ni duka la Rahma Classic, ambako mita tatu zimeibwa katika matukio tofauti.
Mfanyakazi wa duka hilo, Shamimu Abas, alisema walipofika kazini walikuta maji yameingia ndani baada ya mita kuondolewa. Hali hiyo iliwalazimu kusafisha duka na kuokoa bidhaa zao.
“Tumekuja asubuhi tukakuta maji yameingia ndani ya duka. Tumeibiwa mita tatu; jana ilivunjwa moja na leo zimemaliziwa mbili. Tatizo hili lipo pia kwenye nyumba na maduka ya jirani,” alisema Shamimu.
Mkazi mwingine wa Gangilonga, Felista Kagwaro, alisema wananchi hawajui wachukue hatua gani kulinda mita zao, hivyo mamlaka husika zinapaswa kutoa mwongozo na kutafuta suluhisho la kudumu.
“Jana kulikuwa na mafuriko, leo mita zinaibiwa. Tunaomba Serikali ituangalie kwa mkono wa pekee kwa sababu hatujui tuweke walinzi wetu au tufanye nini ili kulinda mita hizi,” alisema Kagwaro.
Katika baadhi ya maeneo, kuondolewa kwa mita kumesababisha maji kutiririka bila kupimwa. Wananchi wamelazimika kutumia uwezo wao kuziba sehemu hizo ili kuzuia upotevu wa maji na uharibifu zaidi.
Kufuatia malalamiko hayo, IRUWASA imetangaza zawadi ya Sh 500,000 kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa wizi huo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa IRUWASA, Restituta Sakila, alisema mamlaka hiyo inawatahadharisha wadau na wakazi wote wa Manispaa ya Iringa kuhusu kuwapo kwa wimbi kubwa la wizi wa mita za maji katika maeneo mbalimbali.
Aliwaomba wananchi kushirikiana na IRUWASA kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kubainika na kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na wizi au uharibifu wa miundombinu ya maji.
“Zawadi nono ya Sh 500,000 itatolewa kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao,” alisema Sakila.
Wananchi wenye taarifa wametakiwa kupiga simu bila malipo kupitia namba 0800 110 122 au 0713 353 695.
Sakila alisema IRUWASA, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, inaendelea na msako wa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote wanaojihusisha na wizi au hujuma dhidi ya miundombinu ya mamlaka hiyo.











0 Comments