Na Matukio Daima Media ,Dodoma
Waandishi wa habari za mazingira nchini, wametakiwa kuandika kwa kina habari za uchunguzi juu ya mambo yanayoendelea nchini ambayo yanachangia athari za mabadiliko ya tabia nchini ili kuokoa jamii.
Maeneo mengi nchini, yanaendelea kuathirika na athari ya mabadiliko ya tabia nchi, kutokana na kuendelea ukataji wa miti, upanuzi wa mashamba maeneo yaliyohifadhiwa, uvamizi wa vyanzo vya maji, uchafu wa mazingira, uvamizi wa maeneo ya nyanda za malisho na uchimbaji madini ambayo haujali athari za kimazingira.
Mhariri mwandamizi wa habari za mazingira, Deodatus Mfugale akitoa mada ya habari za uchunguzi wa mazingira, katika mafunzo ya wanahabari 35 wa mikoa ya kanda ya kati, jijini Dodoma, mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu(THRDC) na Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni(MAIPAC) kwa udhamini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO).
Mfugale alisema,Wanahabari wana nafasi ya kuokoa jamii juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchini, kwa kuandika na kuibua mambo ambayo yanachochea uharibifu wa mazingira kwa kutumia kwa usahihi na kutumia takwimu sahihi, sheria na hivyo kuibua uwajibikaji .
"Waandishi nendeni mkaandike habari za uchunguzi kusaidia jamii ili kuifanya dunia kuendelea kuwa salama lakini muandike kwa usahihi na kujumuisha sauti za wananchi wanaoathirika"anasema.
Mkurugenzi mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma akitoa mada ya msingi wa habari za mazingira alisema mwandishi wa habari za mazingira anapaswa kuandika kwa usahihi,kuandika kwa uhuru,kuelewa maudhui ya jambo ambalo anataka kuliandika, kushirikisha sauti za makundi yote katika jamii ikiwepo Wanawake, vijana, kuleta uwajibikaji na kutetea maslahi ya umma.
Juma alisema wanahabari wanapaswa kuchunguza zaidi athari za mabadiliko ya tabia nchi, katika maeneo mbalimbali, ambazo zimetokana na ongezeko la joto duniani,Ukame, Mafuriko,upungufu wa uzalishaji wa chakula,uharibifu wa ikolojia.
Naye Mkurugenzi wa Mkurugenzi wa Miradi na Uendeshaji wa (THRDC), Wakili Halima Sonda akizungumzia Ukatili dhidi ya waandishi wa habari wanawake, alitaka wanahabari wanawake wapewe fursa sawa na waume katika kuandika habari za uchunguzi za mazingira.
Hata hivyo, alisema kumekuwep udhalilishaji wa wanawake mitandaoni,mifumo dume katika jamii mambo ambayo yanapaswa kupingwa kwani tayari kuna sheria kadhaa, zinazopinga ukatili dhidi ya wanawake na wanahabari wanawake wa mazingira wanapaswa kuzijua .
Mafunzo hayo kwa waandishi kanda ya Kati, kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Iringa, Morogoro ni mfululizo wa mafunzo yanayotolewa na THRDC na MAIPAC kwa wanahabari nchini kupitia mradi wa kuwezesha waandishi wa habari za mazingira kuimarisha uwezo wa wanahabari ili kuchangia uwajibikaji wa mazingira na kukuza uelewa katika jamii tayari mafunzo yametolewa kanda ya kaskazini na Kanda ya Ziwa.












0 Comments