Header Ads Widget

WAGONJWA HOSPITAL TEULE NGAZI YA MKOA TOSAMAGANGA WAFURAHIA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA

 

NA.MATUKIO DAIMA MEDIA .

IRINGA.

Kambi maalum ya madaktari bingwa iliyopo Hospitali teule ngazi ya mkoa   Tosamaganga  wilaya ya Iringa Mkoani Iringa imeendelea kutoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi mkoani Iringa, ikiwa na lengo la kupunguza gharama na usumbufu wa wananchi kusafiri nje ya mkoa kufuata huduma za kibingwa.


Kambi hiyo ambayo  imewakutanisha madaktari bingwa kutoka maeneo mbalimbali, wenye ujuzi na uzoefu katika kada tofauti za afya, huku wananchi wakipata fursa ya kuonana na wataalamu hao na kufanyiwa vipimo pamoja na matibabu.

Akizungumza Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dkt. Athuman  Kihara, alisema kambi hiyo imeanza mwanzoni mwa wiki na inatarajiwa kutoa huduma hadi mwisho wa wiki, huku wananchi wakinufaika na huduma za madaktari bingwa katika maeneo mbalimbali.

Alisema huduma zinazotolewa ni pamoja na magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya mfumo wa mkojo, masikio, pua na koo, usikivu, magonjwa ya ndani, moyo, mfumo wa chakula, mifupa, upasuaji pamoja na magonjwa ya mfumo wa fahamu.

 Dkt. Kihara alisema huduma zinazopatikana katika hospitali hiyo zinatolewa kwa gharama zinazozingatia viwango vilivyowekwa kwa hospitali za Serikali, jambo linalosaidia kupunguza mzigo wa wananchi ambao awali walilazimika kutumia fedha kwa usafiri na malazi wanapokwenda kutafuta huduma nje ya mkoa.


Alisema wananchi wanaokwenda mikoa ya mbali kwa ajili ya matibabu hukabiliwa na gharama za nauli, malazi, chakula na huduma za afya, hivyo upatikanaji wa madaktari bingwa karibu na maeneo yao unawasaidia kutumia fedha kidogo na kupata huduma kwa wakati.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Radiolojia na Mkuu wa Idara ya Radiolojia Dkt Simon Madatula  alisema uwepo wa kambi hiyo umeongeza fursa kwa wananchi wa Iringa na mikoa jirani kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia wataalamu na vifaa vya kisasa.


Alisema Idara ya Radiolojia ina mashine za kisasa zinazowezesha kufanya uchunguzi kwa usahihi na ubora, hali ambayo imepunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri kwenda Dodoma, Mbeya na maeneo mengine kutafuta huduma hizo.


Aliongeza kuwa hospitali hiyo pia ina vifaa vya ultrasound vinavyotumika kufanya vipimo mbalimbali kulingana na mahitaji ya wagonjwa na maelekezo ya madaktari, huku uwepo wa wataalamu wenye ujuzi ukiwezesha matokeo ya vipimo kusomwa na kutafsiriwa kwa usahihi.


Katika huduma za macho, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho, Dkt. Jovin  Nsagale, alisema timu yao imekuwa ikitoa uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ya macho, huku ndani ya siku nne ikiwa imehudumia takribani wagonjwa 88.

Dkt. Nsagale alisema dalili zinazopaswa kumfanya mtu kufika kwa daktari wa macho ni pamoja na kuona ukungu, maumivu ya macho, machozi au uchafu mwingi, jeraha la jicho na mabadiliko ya uwezo wa kuona, huku akiwataka pia watu wenye kisukari na shinikizo la damu kupima macho mara kwa mara.


“Niwashauri  wananchi kuacha kutumia dawa za macho bila ushauri wa wataalamu, pamoja na kutumia miwani ambayo haijaandaliwa baada ya kufanyiwa vipimo, kwa sababu kila mtu ana tatizo na mahitaji tofauti ya macho”alisema


Alisema baadhi ya magonjwa ya macho yanaweza kujificha bila kuonyesha dalili mapema, hivyo wananchi wanapaswa kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara ili matatizo yabainike mapema na kupata matibabu sahihi.

Kwa upande wake mmoja wa wagonjwa waliofika katika kambi hiyo Alfred Ngao kutoka wilaya ya Mufindi alisema kuwa amefika katika kambi hiyo amesema uwepo wa wataalamu hao ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za afya na umeendelea kuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa madaktari bingwa.

TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII

“Tunauomba uongozi wa hospitali kuendelea kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi ili kuwapunguzia gharama za kwenda nje ya mkoa kutafuta huduma hizo jambo ambalo wananchi wengi hawawez kumudu gharama hizo”alisema


Kaimu mkurugenzi wa Hospital hiyo Dkt Thom Malongo alisema kuwa ujio wa madaktari hao ni fursa kubwa kwa wagonjwa kupata huduma .

Pia alisema Hospital hiyo imejipanga kuendelea kuleta madaktari bingwa mara kwa mara ili kuwezesha wananchi wenye uhitaji wa madaktari bingwa kupata huduma hiyo 


TAZAMA TAARIFA YA HABARI BOFYA HAPA

 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI