Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
USHIRIKIANO kati ya Serikali na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) umeelezwa kuwa nguzo muhimu katika kuongeza thamani ya mazao, kukuza viwanda vya usindikaji na kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, katika banda la TADB kwenye Maonesho ya 33 ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Chongolo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kifedha ili kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji kupata mitaji itakayoongeza uzalishaji, kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais alipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa TADB, Mkani Waziri, kuhusu huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo kwa wadau wa sekta ya kilimo na namna zilivyochangia kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Aidha, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Kula cha Trolle Meesle, Daniel Amulike, amesema ufadhili wa TADB umeiwezesha kampuni hiyo kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula kutoka tani 30 hadi tani 624 kwa mwezi baada ya kujenga kiwanda cha kisasa.
Amesema ongezeko hilo limeongeza uwezo wa kampuni kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Dkt. Nchimbi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Siku ya Tatu ya Maonesho hayo alijionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na TADB katika kuwawezesha wadau wa sekta ya kilimo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uzalishaji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.












0 Comments