Header Ads Widget

EWURA YARAHISISHA UWEKEZAJI WA VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI ILI KUDHIBITI BIASHARA HOLELA.

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea kurahisisha masharti ya uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini kwa kupunguza gharama za leseni na kurahisisha vigezo vya ujenzi, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za mafuta na kudhibiti biashara holela ya uuzaji wa mafuta.

Akizungumza na waandishi wa habari katika         maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongoro, Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira, amesema mamlaka hiyo imepunguza ada ya maombi ya leseni kutoka shilingi milioni tano hadi shilingi milioni moja kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini ili kuhamasisha uwekezaji katika maeneo ambayo bado hayana huduma hiyo.

"Watu wengi wanafikiri uwekezaji wa vituo vya mafuta unahitaji mtaji mkubwa, lakini EWURA imeweka utaratibu maalumu wa kurahisisha uwekezaji katika maeneo ya vijijini. Gharama ya maombi ya leseni imepunguzwa kutoka shilingi milioni tano hadi milioni moja," amesema Musira.

Ameeleza kuwa pamoja na kupunguza gharama za leseni, EWURA imerahisisha masharti ya miundombinu kwa kuruhusu vituo vya mafuta vya vijijini kuwa na pampu moja au kuuza aina moja ya bidhaa ya mafuta kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Musira amesema pia wawekezaji wa maeneo ya vijijini wanaruhusiwa kutumia vibali  vya mazingira vinavyotolewa na maafisa mazingira wa halmashauri husika, huku maeneo ambayo hayajapimwa rasmi yakitambuliwa endapo mwekezaji atawasilisha kibali kutoka kijiji au mtaa kinachoruhusu ujenzi wa kituo cha mafuta.

Amesema hatua hizo zinalenga kuondoa biashara isiyo rasmi ya uuzaji wa mafuta katika chupa na vidumu, ambapo inaweza kuwa hatari  kwa maisha ya wananchi na  mali zao kutokana na bidhaa hiyo kutokuwa rafiki kwa mazingira ya vijijini hivyo inaweza kusababisha athari.

"Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mafuta kwa usalama kupitia vituo vinavyotambulika kisheria badala ya kuendelea kununua mafuta yanayouzwa kiholela," amesema" Musira.

Aidha amefafanua kuwa EWURA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake, kupokea malalamiko ya watumiaji pamoja na kuwahamasisha wawekezaji kuwekeza katika sekta zinazosimamiwa na mamlaka hiyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI