Header Ads Widget

TEKNOLOJIA YAIBUA VIVUTIO VYA ASILI, TFS YAWAKARIBISHA WATANZANIA UTALII WA KIDIJITALI


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

DODOMA — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetumia teknolojia ya kisasa kuwapa wananchi fursa ya kutembelea na kufahamu vivutio vya utalii wa mazingira asilia kwa njia ya kidijitali kabla ya kuvifikia moja kwa moja.

Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma, Meneja wa Kituo cha TFS cha Michoro ya Kondoa Irangi, Zuberi Mabie, amesema teknolojia hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kutangaza vivutio vya asili vinavyosimamiwa na TFS na kuhamasisha utalii wa ndani.

Amesema kupitia huduma ya virtual tour, wananchi wanaweza kupata taswira halisi ya maeneo mbalimbali ya utalii ikiwemo misitu ya asili, mapango, maporomoko ya maji, maeneo ya ikolojia ya kipekee na michoro ya miambani kabla ya kupanga safari ya kuyatembelea.

“Teknolojia hii inasaidia kuwafikisha watu karibu na vivutio ambavyo huenda hawajawahi kuvifahamu. Wananchi wanaweza kuona uzuri wa maeneo haya kidijitali na kupata taarifa sahihi za namna ya kuyafikia,” amesema Mabie.

Amesema Kituo cha Michoro ya Kondoa Irangi kinaendelea kutumia mbinu za kisasa katika kutangaza urithi wa asili, ikiwemo kuwafahamisha wananchi kuhusu thamani ya michoro hiyo ya kihistoria na umuhimu wa kuihifadhi kwa vizazi vijavyo.

Mabie amewataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Nane Nane kutembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ili kupata elimu kuhusu vivutio mbalimbali vinavyosimamiwa na TFS pamoja na kupanga safari za utalii wa ndani.

Ameongeza kuwa tarehe 9 Agosti 2026 kutakuwa na safari maalumu ya utalii wa ndani kuelekea eneo la Michoro ya Miambani Kolo, Kondoa, kwa ajili ya wananchi kupata uzoefu wa moja kwa moja wa urithi huo wa asili.

Amesema utalii wa ndani una mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuongeza uelewa wa uhifadhi na kuimarisha ushiriki wa jamii katika kulinda rasilimali za mazingira.

“Tunawahimiza Watanzania kujifunza na kutembelea vivutio vilivyopo nchini. Kila safari ya utalii ni sehemu ya kuunga mkono uhifadhi na maendeleo endelevu,” amesema Mabie.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI