Taarifa kwa UMMA Kuhusu Uandaaji wa Muswada wa Mfano (Model Bill) wa Kuongoza Mchakato wa Mazungumzo ya Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa
Kamati ya Kusukuma Maridhiano ya Kitaifa (KKMK) inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania, taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, wadau wa maendeleo, vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini pamoja na makundi yote ya kijamii kuwa imeanza rasmi maandalizi ya Muswada wa Mfano (Model Bill) utakaoweka mfumo wa kisheria na kiutawala wa kuendesha Mchakato wa Mazungumzo ya Maridhiano na Muafaka wa Taifa.
Hatua hii inafuatia mapendekezo yaliyotolewa na Jaji Chande kuhusu umuhimu Mazungumzo ya Maridhiano ya kitaifa na Muafaka wa Kitaifa kuponya na kuandaa Taifa kwenda kwenye mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya.
KKMK inaamini kuwa Tanzania ina wajibu wa kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kuendeleza misingi ya haki, usawa, maridhiano na demokrasia jumuishi kupitia mazungumzo yenye kujenga uelewano wa kitaifa na kuimarisha amani ya kudumu.
Muswada huo wa Mfano unatarajiwa:
1) Kuweka mfumo rasmi wa uendeshaji wa Mazungumzo ya Maridhiano na Muafaka wa Taifa ikiwemo Uteuzi wa Wajumbe,Ajenda za Mazungumzo, Muundo wa Tume nk
2) Kufafanua wajibu wa wadau mbalimbali katika mchakato wa maridhiano;
3) Kuweka misingi ya ushirikishwaji wa wananchi na taasisi mbalimbali;
4) Kuweka taratibu za utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa;
5) Kulinda misingi ya haki, uwazi, uwajibikaji na umoja wa kitaifa.
6) Fidia kwa Waathirika
Katika kuandaa Muswada wa Mfano huo, KKMK itafanya mashauriano mapana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa maoni ya wananchi na makundi yote yanazingatiwa kikamilifu.
KKMK inatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kwa amani, uwazi na uzalendo katika kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kujenga Taifa lenye mshikamano, haki na maridhiano ya kudumu.
Kamati pia inapenda kusisitiza kuwa mchakato huu si wa kisiasa pekee, bali ni agenda ya kitaifa inayolenga kuimarisha umoja wa taifa, kulinda amani na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Ratiba ya mashauriano na namna ya kuwasilisha maoni itatangazwa rasmi kupitia vyombo mbalimbali vya habari na majukwaa ya umma.
Imetolewa na:
Odero Charles Odero
Mwenyekiti Kamati Kusukuma Maridhiano ya Kitaifa (KKMK)







0 Comments