Na Mwandishi Wetu, Nairobi
NAIROBI: Tanzania imezitaka nchi duniani kuimarisha ushirikiano, kuongeza fedha na kuharakisha uhamishaji wa teknolojia ili kufanikisha Muundo wa utekelezaji wa Kunming-Montreal wa Baioanuai (KMGBF), ikisema hatua hizo ni muhimu kuzuia kuendelea kwa uharibifu wa baioanuai ifikapo mwaka 2030.
Msimamo huo uliwasilishwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kwa niaba ya jopo la wataalam wa Mazingira wa Tanzania Fandey H. Mashimba, katika Mkutano wa Saba wa Chombo Tanzu cha Utekelezaji (SBI-7) chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Baioanuai (CBD), unaofanyika Nairobi, Kenya. Tanzania pia iliunga mkono tamko la Ghana lililotolewa kwa niaba ya Kundi la Afrika (African Group).
Mashimba alisema Tanzania imeendelea kutekeleza malengo ya KMGBF kupitia Mkakati na Mpango wa Taifa wa Baioanuai (NBSAP), huku ikiimarisha uhifadhi wa misitu na maeneo yenye utajiri mkubwa wa baioanuai (biodiversity hotspot), wanyamapori, bahari na ukanda wa pwani, pamoja na kurejesha mifumo ya ikolojia kwa kushirikisha jamii.
Alisema juhudi hizo zinafanyika Tanzania Bara na Zanzibar, zikihusisha maeneo yenye mifumo muhimu ya kiikolojia kama vile misitu ya Miombo na mbuga (savannah) maeneo oevu, mikoko, miamba ya matumbawe, milima na visiwa vyenye utajiri mkubwa wa baioanuai.
Hata hivyo, Tanzania ilisema mafanikio ya utekelezaji wa muundo huo yatategemea upatikanaji wa fedha za uhakika, ushirikiano wa kisayansi, ujenzi wa uwezo na kuboreshwa kwa mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za baioanuai.
Aidha, ilizitaka taasisi za kimataifa kuongeza msaada kwa nchi zinazoendelea kupitia Mfuko wa Muundo wa utekelezaji wa Kimataifa wa Baioanuai (Global Biodiversity Framework Fund–GBFF) pamoja na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (Global Environment Facility–GEF) ili ziweze kutekeleza kwa ufanisi malengo ya mkataba huo.
Tanzania pia ilisisitiza kuwa tathmini za kimataifa zinapaswa kuzingatia mazingira na uwezo wa kila nchi, badala ya kutafsiri upungufu wa takwimu kuwa ushahidi wa utekelezaji dhaifu.
Akihitimisha tamko hilo, Mashimba alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Mkataba wa Baioanuai kuhakikisha malengo ya Muundo wa Kunming-Montreal yanafikiwa ifikapo mwaka 2030.







0 Comments