Header Ads Widget

MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA YATAJWA KUWA NGUZO UMUHIMU UZALISHAJI WA MAZAO


Afisa Biashara kutoka kiwanda cha FOMI  Hellen Kasika, akiwa katika moja ya shamba darasa la zao la pamba walilotumia mbolea ya FOMI


Bwana Shamba  kutoka FOMI Melkior Pius Tanda wa pili kutoka kushoto akiwa na baadhi ya wakulima waliofika katika shamba darasa kujifunza
Moja ya shamba darsa lililoandaliwa katika kwa kutumia mbolea ya FOMI katika viwanja vya nanenane nyamhongoro kwa ajili wakulima kujifunza

Bwana Shamba kutoka kiwanda cha kutengeneza mbolea ya FOMI Melkior Pius Tanda akiwa katika moja ya shamba darasa na kuonesha namna mbolea ya FOMI inavyoweza kutumika na kuleta tija katika mazao.

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Matumizi sahihi ya mbolea yameelezwa kuwa nguzo muhimu katika kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha kipato cha wakulima, huku wataalamu wa kilimo wakisisitiza kuwa pamoja na upatikanaji wa pembejeo, elimu ya namna ya kutumia mbolea kwa kuzingatia hatua za ukuaji wa mazao ndiyo inayobeba mafanikio ya mkulima.

Wito huo umetolewa na wataalamu wa kiwanda  cha Itracom Fertilizers Limited (FOMI) katika Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza, ambapo wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea zinazochangia kuongeza tija ya uzalishaji huku zikihifadhi afya ya udongo.

Akizungumza katika maonesho hayo, Bwana Shamba kutoka kiwanda cha Itracom Fertilizers Limited, Melkior Pius Tanda, alisema mbolea ni chakula cha mmea, hivyo mkulima anapaswa kuitumia kwa usahihi ili mmea upate virutubisho vinavyohitajika katika kila hatua ya ukuaji wake.

"Tunamshauri mkulima kutumia mbolea kwa sababu ni chakula cha mmea unapoweka mbolea unaulisha mmea wako na kuuwezesha kutoa mavuno yenye tija, Mbolea za FOMI zina mchanganyiko wa samadi na virutubisho vya madini unaosaidia kulinda afya ya udongo, kuhifadhi unyevunyevu na kufanya mmea upate virutubisho kwa muda mrefu," alisema Tanda.

Tanda ameeleza kuwa kampuni hiyo inazalisha aina 14 za mbolea zinazotumika katika hatua mbalimbali za ukuaji wa mazao, zikiwemo FOMI Otesha kwa kupandia, FOMI Kuzia kwa kukuzia, FOMI Nenepesha kwa hatua ya kunenepesha mazao, pamoja na mbolea maalumu kwa mazao ya miwa, tumbaku, chai na kilimo cha asili.

Naye Afisa Biashara wa kampuni hiyo, Hellen Kasika, alisema FOMI imekuwa ikitumia maonesho ya Nanenane, Siku ya Mbolea Duniani na maafisa ugani waliopo katika wilaya mbalimbali kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima.

"Mkulima anatakiwa kuanza na mbolea ya kupandia wakati wa kupanda, kisha baada ya siku 14 hadi 21 aweke mbolea ya kukuzia. Kutofuata utaratibu huo kunaweza kupunguza ufanisi wa mbolea na mavuno yanayotarajiwa," alisema Kasika.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo imeanzisha mashamba darasa katika maeneo mbalimbali nchini ili wakulima wajifunze kwa vitendo namna sahihi ya kutumia mbolea na kujionea matokeo yake mashambani.

Kwa upande wake, mkulima kutoka Wilaya ya Kwimba, Ndohele Innocent, alisema elimu aliyoipata kutoka banda la FOMI imemfungua macho kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, akibainisha kuwa hapo awali alikuwa akitumia mbolea bila kuelewa tofauti ya mbolea ya kupandia, kukuzia na kunenepesha mazao.

"Sisi wengi tulikuwa tunanunua mbolea moja na kuitumia kwa kila hatua ya ukuaji wa zao, baada ya kupata elimu hapa nimeelewa kuwa kila mbolea ina matumizi yake elimu kama hii iwafikie wakulima wengi ili tuongeze uzalishaji," alisema Innocent.

Aidha alitoa wito kwa wasambazaji wa mbolea nchini kuendelea kuwapa wakulima elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo wanapozinunua ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kuhakikisha uwekezaji wa wakulima unaleta matokeo yanayokusudiwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI