Header Ads Widget

TIRDO YALEA UBUNIFU WA VIWANDA, YASUKUMA TEKNOLOJIA ZA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO


Na Matukio DaimaMedia 

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limesema linaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya viwanda kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, hatua inayolenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa na kuongeza kipato kwa wakulima na wajasiriamali.


Akizungumza katika Maonyesho ya Nanenane 2026,Mtaalam na Mtafiti wa Teknolojia za Nishati, Mhandisi Augustino Masse kutoka TIRDO alisema shirika hilo linaimarisha mnyororo wa thamani wa mazao kupitia utafiti, ubunifu na teknolojia zinazosaidia mazao kudumu kwa muda mrefu bila kupoteza ubora wake.


Alisema kuwa, tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya mazao yanayoharibika kwa haraka, yakiwemo nyanya, matunda na mboga za majani, hupotea kutokana na ukosefu wa teknolojia sahihi za uhifadhi na usindikaji.


Kutokana na hali hiyo, TIRDO imeendelea kuhamasisha matumizi ya makaushio yanayotumia nishati ya jua (solar dryers), teknolojia inayowezesha mazao kukauka kwa viwango vinavyokubalika huku yakihifadhi ubora, virutubisho na kuongeza muda wa kuhifadhi.


Mhandisi Masse alisema kila zao lina mahitaji yake ya kitaalamu katika mchakato wa ukaushaji, hivyo TIRDO imebuni makaushio yanayozingatia kiwango cha joto na muda unaohitajika kwa kila zao ili kuhakikisha ubora wa bidhaa unaendelea kubaki.

Mbali na teknolojia za ukaushaji, alisema shirika hilo linaendelea kuhimiza matumizi ya nishati mbadala kwa kuhamasisha mabaki ya mazao ya kilimo kutumika kuzalisha nishati, hatua inayosaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa pamoja na kuhifadhi mazingira.


Alibainisha kuwa TIRDO tayari imewezesha ujenzi wa makaushio zaidi ya saba katika maeneo mbalimbali nchini, huku mradi mwingine ukiendelea kutekelezwa Mbagala jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa Mhandisi Masse, jukumu la TIRDO si kutengeneza bidhaa kwa ajili ya kuziuza sokoni, bali ni kulea na kuendeleza wabunifu na wajasiriamali kwa kuwapatia ushauri wa kitaalamu, teknolojia na mbinu za uzalishaji ili bidhaa zao zikidhi viwango vya ubora kabla ya kuwasilishwa kwa mamlaka za udhibiti na uthibitishaji kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS).


Aliongeza kuwa kupitia huduma za incubation, TIRDO imeendelea kuwajengea uwezo wabunifu wengi wa Kitanzania kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa zenye thamani ya kibiashara, hatua inayochochea ukuaji wa viwanda na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.


Aidha, aliwataka wakulima, wajasiriamali na wananchi wanaotembelea Maonyesho ya Nanenane 2026 kutembelea banda la TIRDO ili kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo, zikiwemo za kuongeza thamani ya mazao, matumizi ya nishati mbadala na fursa za kulea bunifu zinazoweza kugeuka kuwa biashara zenye tija.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI