Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media
TANZANIA imeendelea kung'ara barani Afrika katika sekta ya mbegu baada ya kushika nafasi ya tatu kati ya nchi 55 kwa ubora wa mifumo ya mbegu, huku Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) ikiongeza kasi ya mapambano dhidi ya mbegu feki na zisizokidhi viwango ili kulinda wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimangu, amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarishwa kwa ukaguzi katika maduka ya mbegu, maghala na viwanda vya kuchakata mbegu kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya wahusika 22 waliokiuka Sheria ya Mbegu walichukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani, kutozwa faini na kuwalipa fidia wakulima walioathirika na mbegu zisizokidhi viwango.
"Tanzania imepata alama 7.25 kati ya 10 katika tathmini ya The African Seed Access Index (TASAI) 2023, na kushika nafasi ya tatu barani Afrika nyuma ya Afrika Kusini iliyopata alama 8.62 na Zambia yenye alama 7.89.", Amesema
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa na uimara wa sheria na sera za mbegu, ubora wa vifungashio, uidhinishaji wa aina mpya za mbegu, mifumo ya mbegu inayosimamiwa na wakulima, pamoja na kuimarika kwa biashara ya mbegu ndani na nje ya nchi.
Mbali na mafanikio hayo, Tanzania imeendelea kudumisha ithibati ya International Seed Testing Association (ISTA) na kuwa miongoni mwa nchi 14 za Afrika na 80 duniani zenye maabara zilizoidhinishwa kimataifa kupima ubora wa mbegu.
Chimangu amesema ithibati hiyo imeiwezesha Tanzania kutoa vyeti vya ISTA Orange International Certificate (OIC) kwa mbegu zinazouzwa nje ya nchi, hatua iliyovutia kampuni za kimataifa za uzalishaji na biashara ya mbegu, ambazo sasa zinafikia takribani 29 nchini.
Aidha, Tanzania imeendelea kuwa mwanachama wa Skimu za Mbegu za Shirika la OECD, ikiwa miongoni mwa nchi 10 za Afrika zinazoshiriki katika mfumo huo wa kimataifa, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani wa mbegu za Tanzania katika soko la dunia na kupanua fursa za biashara.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, TOSCI ilitoa vibali 392 vya kusafirisha nje ya nchi tani 993.21 za mbegu. Kati ya hizo, tani 722.20 zilikuwa mbegu za mikunde, tani 204.07 za nafaka, tani 55.44 za mazao ya bustani na tani 11.50 za mazao ya mafuta, hali inayoonyesha kuimarika kwa uzalishaji na mauzo ya mbegu za Tanzania katika masoko ya kimataifa.







0 Comments