Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma
JESHI la Polisi nchini limesema litaendelea kuimarisha ulinzi na usalama huku likiongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali za kipolisi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya jeshi hilo na jamii katika kudhibiti uhalifu.
Hayo yameelezwa na mwakilishi wa Jeshi la Polisi katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dk. John Samuel Malecela jijini Dodoma, ambapo amesema jeshi hilo limetumia maonesho hayo kuwafikia wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu majukumu yake pamoja na huduma zinazotolewa katika vituo vya polisi.
Amesema uwepo wa Jeshi la Polisi katika maonesho hayo unatokana na wajibu wake wa kikatiba na kisheria wa kulinda amani, usalama wa raia na mali zao, kusimamia utekelezaji wa sheria, kupeleleza makosa ya jinai pamoja na kuwakamata wahalifu.
Amesema Mkoa wa Dodoma unaendelea kuwa salama kutokana na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na jeshi hilo ikiwemo kuimarisha doria, misako na operesheni maalumu ndani na nje ya viwanja vya maonesho ili kuhakikisha wananchi na wageni wanashiriki shughuli hizo kwa utulivu.
"Mbali na kutoa huduma za ulinzi, tumeandaa mabanda maalumu kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali za kipolisi ili wananchi wafahamu taratibu za kupata huduma wanapofika katika vituo vya polisi," amesema.
Amesema elimu inayotolewa inahusu Chumba cha Mashtaka, Dawati la Polisi Jamii, Polisi Mtandao, Kitengo cha Alama za Vidole (Fingerprints), usalama barabarani, udhibiti wa madawa ya kulevya, makosa ya mtandao, haki za binadamu, Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto, pamoja na Kitengo cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STU).
Pia amesema wananchi wanapata elimu kuhusu Kitengo cha Polisi Mazingira, Madini na Maliasili, matumizi salama ya silaha, madhara ya umiliki haramu wa silaha pamoja na shughuli za Kitengo cha Ushirikishwaji Jamii.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limesema linaendelea kushirikiana na waganga wa tiba asili walioshiriki maoneshoni kwa kuwahimiza kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria za nchi na kuepuka matumizi ya ramli chonganishi.
Aidha, limewataka waganga hao kutoa taarifa kwa vyombo vya dola endapo watabaini watu wanaowafuata kwa lengo la kujikinga dhidi ya makosa ya jinai waliyoyafanya au wanayokusudia kuyafanya.
Hata hivyo Jeshi la Polisi limewashukuru wananchi waliotembelea banda lake katika Maonesho ya Nanenane na kuwahimiza kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kuendelea kudumisha amani, usalama na utulivu nchini.











0 Comments