Na Matukio Daima Media, Dar es salaam
UMOJA wa Wataalamu wa Tiba Asilia Tanzania (UMAWATI) umewataka Watanzania kuendelea kuthamini na kulinda tiba asilia, ukieleza kuwa licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, matumizi ya dawa za mitishamba bado yana mchango mkubwa katika sekta ya afya.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa kutangaza maadhimisho ya miaka minne ya Kituo Kikuu cha Huduma za Tiba Asilia na Matambiko Afrika Mashariki na Kati.
Umoja wa Wataalamu wa Tiba Asilia Tanzania, UMAWATI, unasema ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kuthamini urithi wa tiba asilia ulioachwa na mababu, badala ya kuupuuza kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa UMAWATI, Dkt. Riziki Malela, amesema dawa za mitishamba zina nafasi muhimu katika tiba, akibainisha kuwa hata baadhi ya dawa zinazotumika hospitalini zimetokana na tafiti za mimea na mitishamba.
Akasema tusipoenzi asili ya mtanzania na kukumbuka tutokapo, tutapoteza hazina kubwa ambayo vizazi vilivyopita viliiacha.
Akaongeza kuwa hata nyingi zinazotumika hospitalini zimetokana na mitishamba, hivyo ni muhimu kuendelea kuithamini tiba huyo asilia.
Katika hatua nyingine, UMAWATI imebainisha uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya miaka minne ya Kituo Kikuu cha Huduma za Tiba Asilia na Matambiko Afrika Mashariki na Kati, yatakayofanyika kuanzia Agosti 15 hadi 17, 2026 katika Kijiji cha Kibindu, Wilayani Chalinze, mkoani Pwani, yakitarajiwa kuhudhuriwa na wageni kutoka mataifa mbalimbali Duniani.
Mkuu wa Idara ya Uzalishaji wa Nje Maulidi Janga, akawataka wataalamu wote wa tiba asilia kuhakikisha wanasajiliwa kisheria kabla ya kutoa huduma kwa wananchi.
Akawakumbusha wataalamu wote wa tiba asilia ambao bado hawajasajiliwa kufanya hivyo mara moja kwani kutoa huduma bila usajili ni kinyume cha sheria na hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yao.
UMAWATI imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha utafiti, matumizi salama ya tiba asilia na ufuataji wa sheria ili sekta hiyo iendelee kutoa mchango katika kuboresha afya za Watanzania.










0 Comments