Header Ads Widget

FDH, STAMICO KUSAINI MAKUBALIANO NA CHUO CHA MAFUNZO ZANZIBAR

 

 Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

FOUNDATION for Disabilities Hope (FDH) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kesho Agosti 11, 2026, zinatarajia kusaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo cha Mafunzo Zanzibar, hatua inayolenga kuimarisha usambazaji wa mkaa mbadala wa Rafiki Briquette na kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.

Mkurugenzi wa FDH, Maiko Salalia, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kukuza matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira, huku FDH ikipewa jukumu la kushiriki katika usambazaji na uuzaji wa mkaa huo mbadala kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Salalia amesema FDH imekuwa ikifanya mazungumzo na taasisi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha Rafiki Briquette inawafikia wananchi kwa wingi na kwa urahisi.


Amesema ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa mpya katika usambazaji wa mkaa mbadala, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza matumizi ya nishati chafu na kulinda mazingira.

“Kesho tutakuwa na tukio kubwa la kihistoria la kusaini makubaliano ya ushirikiano baina ya Chuo cha Mafunzo Zanzibar na STAMICO, kwa kushirikiana na FDH, katika usambazaji mkubwa wa mkaa mbadala wa Rafiki Briquette,” amesema.


Salali amesema FDH tayari imekabidhiwa cheti cha uwakala wa mkaa huo, hatua ambayo imeipa taasisi hiyo msukumo wa kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa agenda ya nishati safi.


Amesema mkaa huo mbadala unalenga kuwasaidia Watanzania kupata nishati rafiki kwa mazingira na kupunguza utegemezi wa nishati zinazochangia uharibifu wa mazingira.

“Tunajivunia sana utekelezaji wa agenda hii ya nishati safi na tunajivunia STAMICO kwa kuja na mkaa mbadala ambao unaenda kusaidia utunzaji wa mazingira na kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati chafu,” amesema.


Ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mazingira na kujenga mazingira bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI