Header Ads Widget

VETA NJIRO YAJA NA UBUNIFU HUU SABASABA

 

Na Matukio DaimaMedia 

Chuo cha Ufundi Stadi Tanzania (Veta) Njiro, Arusha, kimetumia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuonyesha ubunifu wa utengenezaji wa vyakula vinavyozingatia afya kwa kutumia mazao ya asili, huku kikitoa wito kwa vijana kutumia mafunzo ya ufundi kujiajiri.


Akizungumza katika maonesho hayo, Mwalimu wa uandaaji na upikaji wa vyakula kutoka Veta Njiro, Robinson Fomokuju, alisema chuo hicho kinafundisha namna ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwa kuyageuza kuwa bidhaa zinazoweza kuuzwa sokoni.


Alisema badala ya kutegemea unga wa ngano pekee, wanafundisha matumizi ya unga wa muhogo, ndizi, mbaazi, maharage na korosho kutengeneza mikate, keki na bidhaa nyingine zenye lishe bora.

"Tunataka kuwaonyesha Watanzania kwamba mazao yetu yanaweza kuongezewa thamani na kutengenezwa bidhaa mbalimbali zinazoweza kuleta kipato, huku zikichangia afya bora," alisema.


Fomokuju alisema banda la Veta linaonyesha bidhaa mbalimbali ikiwemo mikate ya muhogo, keki zisizotumia sukari, keki za maharage (protein cake), pamoja na bidhaa nyingine zinazotokana na mazao ya ndani.

Alisema pia chuo hicho kinaanza kutekeleza sera ya kuimarisha mafunzo ya ujuzi kwa vijana, akitolea mfano mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba ambaye tayari amewezeshwa kupata ujuzi wa kutengeneza bidhaa hizo.


Aidha, amewahimiza vijana waliomaliza shule na ambao hawajapata nafasi ya kuendelea na elimu ya juu kujiunga na Veta kwa mafunzo ya muda mfupi au muda mrefu ili kujipatia ujuzi wa kujiajiri.


"Fursa bado zipo. Ada za Veta ni nafuu na mafunzo tunayotoa yanamwezesha kijana kujiajiri na kuongeza kipato chake," alisema.


Alitoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Veta katika maonesho hayo ili kujionea ubunifu wa bidhaa zinazotokana na mazao ya Tanzania na kupata elimu kuhusu fursa za mafunzo ya ufundi stadi.


Kwa upande wake, Said Shauri ambae ni mwanafunzi wa veta Arusha, amesema kuwa, matokeo ya darasa la saba hayakua mabaya hata kidogo lakini aliamua kusomea mapishi kwa sababu ni kitu ambacho anapenda kukifanya .


Amesema kuwa, alipomueleza mama yake alimkubalia mara moja na kumpeleka katika shule ya Veta Aruusha, ambako sasa anasoma na kufundishwa vizuri kiasi cha kuelewa masomo yake kwa urahisi.


"Nimependa kusomea mapishi kwa sababu nilifaulu vizuri darasa la saba, nilipotoka darasa la saba nikamwambia mama nataka nikasomee mapishi, akanijibu sawa, akanipeleka kwenye shule ya Veta ya Arusha na sasa hivi mwalimu ananifundisha vizuri na ninaelewa vizuri," amesema Said


Ameongeza kuwa Veta ni mahali sahihi kwa vijana waliomaliza shule, waliopata matokeo mazuri au hata wale ambao hawakufanya vizuri, kwa kuwa kuna fursa nyingi za kujifunza ujuzi mbalimbali unaoweza kuwasaidia kujiajiri.


"Nawaambia watoto ambao wako nyumbani, labda wamefeli au wamefaulu vizuri kama mimi na wanataka kufanya kitu fulani lakini wameshindwa, waende kwenye shule ya Veta. Veta ziko miji mingi sana, hata Dar es Salaam zipo nyingi sana. Kuna mafunzo mengi sana," amesema.


Said amesema mafunzo ya mapishi anayopata yamefungua matumaini mapya ya maisha yake na kwamba anaamini ujuzi huo utamsaidia kujitegemea na kuwa na maisha bora baadaye.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI