.
Na Matukio Daima, Morogoro.
Serikali imeielekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuongeza matumizi ya teknolojia katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wanaovamia makazi ya wananchi, huku ikitakiwa kuandaa mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu ya kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
Maelekezo hayo yanatolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TAWA katika Makao Makuu ya mamlaka hiyo mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutathmini utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kijaji ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia yanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya uhifadhi, hususan katika maeneo yanayokumbwa na matukio ya wanyamapori kuvamia makazi ya wananchi na kusababisha madhara kwa maisha na mali.
Amesisitiza kuwa pamoja na kulinda wanyamapori, ni muhimu kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wanakuwa salama, huku akielekeza TAWA kuendelea kushirikisha jamii katika shughuli za uhifadhi kwa kuwa ndiyo walinzi wa kwanza wa rasilimali hizo.
Aidha, Waziri huyo ameipongeza TAWA kwa kuendelea kuvutia wawekezaji katika maeneo ya uhifadhi, hatua iliyosaidia kuongeza mapato ya mamlaka na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, ameeleza kuwa uimarishaji wa ulinzi wa rasilimali za wanyamapori umechangia kuongezeka kwa idadi ya baadhi ya wanyamapori, ikiwemo swala aina ya Puku, pamoja na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji katika maeneo yanayosimamiwa na mamlaka hiyo.
Amesema TAWA imeendelea kusaini mikataba mipya ya uwekezaji, huku maeneo ya uwekezaji mahiri yakiongezeka na kuchangia karibu nusu ya mapato ya mamlaka hiyo
Katika kukabiliana na migongano kati ya binadamu na wanyamapori, Mtaalamu wa Ndege Nyuki wa TAWA, Mhifadhi Juliet Mboko, ameeleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kutumia ndege nyuki kuwazuia tembo na wanyamapori wengine kuingia katika mashamba na makazi ya wananchi.
Naye Afisa Mhifadhi Daraja la Kwanza, Isack Chamba, amesema pamoja na teknolojia hiyo, TAWA imeendelea kutumia doria za mara kwa mara, uzio wa umeme na mbinu nyingine za kisasa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuzuia mifugo kuingia katika maeneo ya hifadhi.
Kwa mujibu wa taarifa ya utendaji iliyowasilishwa mbele ya Waziri, TAWA imekamilisha ujenzi wa mabwawa 14, vizimba 31 na vituo 14 vya askari ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Taarifa hiyo pia imeonyesha kuwa mamlaka imekusanya zaidi ya Sh bilioni 92 hadi Juni mwaka huu, imeongeza idadi ya watalii wa picha wanaotembelea maeneo yake na kuendelea kutoa gawio kwa WMA, vijiji na halmashauri zinazozunguka maeneo ya hifadhi, hatua zinazolenga kuhakikisha uhifadhi unatoa manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Mwisho









0 Comments