Header Ads Widget

KAJENJERE YATUMIA FUNZA KUBADILI TAKA KUWA MBOLEA NA CHAKULA CHA MIFUGO

 

Na Matukio DaimaMedia 

Kampuni ya Kajenjere imesema imebuni mfumo wa kutumia funza maalumu kuchakata taka za kikaboni na kuzigeuza kuwa mbolea pamoja na chakula chenye protini nyingi kwa mifugo, hatua inayolenga kulinda mazingira na kupunguza gharama za ufugaji.


Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), mfanyakazi wa kampuni hiyo, Zakaria, Joseph na mtaalam wa kuzalisha funza kutoka kajenjere alisema teknolojia hiyo hutumia funza maalumu wanaokula mabaki ya chakula, matunda na taka nyingine za kikaboni ambazo mara nyingi hutupwa mazingira.

Alisema mchakato huanza kwa funza hao kutaga mayai, ambayo huanguliwa na kutoa funza wadogo. Baada ya hapo, funza hulishwa taka za kikaboni hadi kuzimaliza.


"Baada ya funza kumaliza kula mabaki ya chakula, tunapata bidhaa mbili muhimu. Tunapata mbolea ya asili na tunavuna funza ambao hutumika kutengeneza chakula cha mifugo," alisema.


Alifafanua kuwa chakula hicho hutumika kwa kuku, samaki, bata, nguruwe na mbwa, huku kikiwa na kiwango kikubwa cha protini kinachosaidia kuboresha afya na ukuaji wa mifugo.



Zakaria alisema tofauti na baadhi ya vyakula vya mifugo vinavyotumia dagaa na malighafi nyingine za baharini, chakula kinachotokana na funza ni mbadala unaosaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza utegemezi wa rasilimali hizo.

Alitoa wito kwa wafugaji kutumia bidhaa hiyo, akisema inaweza kuongeza tija katika ufugaji kutokana na ubora wake wa lishe.

"Tunawahimiza wafugaji kuanza kutumia chakula hiki kwa sababu kina virutubisho vingi na kinachangia mifugo kuwa na afya bora na kuzalisha zaidi," alisema.


Aliongeza kuwa ubunifu huo unasaidia kutatua changamoto mbili kwa wakati mmoja; usimamizi wa taka za kikaboni na upatikanaji wa chakula bora cha mifugo, huku ukichangia uhifadhi wa mazingira.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI