Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Wakazi wa eneo la Katubuka manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma ambao nyumba zao zimezingirwa na maji kwa miaka mitatu wamemuomba Raisi Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kupata msaada utakaowezesha kuendelea na maisha kama kawaida kufuatia athari kubwa ya nyumba zao kuzama kwenye maji.
Wananchi hao wametoa kauli hiyo mbele ya Mkuu wa wilaya Kigoma, Rashid Chuachua kwenye shule ya Msingi Majengo Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo baadhi yao wameamua kuhamia hapo kufuatia mvua za mwishoni mwa wiki hii kuongezeka na nyumba zaidi kuzama kwenye maji.
Mmoja wa waathirika wa mafuriko katika eneo la Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, Bau Khalid Kengwa alisema tatizo la nyumba zao kuingiliwa na maji lilianza mwaka 2023 lakini hadi leo hakuna hatua zozote za serikali kuwasaidia kupata maeneo mengine wakati waliuziwa viwanja na serikali na wana hati.
Naye Nelson Kubila mwananchi mwingine aliyeathirika na nyumba yake kuingiliwa na maji katika eneo hilo alisema kuwa hadi sasa nyumba 165 zenye jumla ya watu Zaidi ya 800 wameathirika tangu mwaka 2023 lakini hawajaona jitihada zozote za serikali katika kuwasaidia kuondokana na janga hilo ambapo alisema kuwa hapo shuleni ambapo wamehamia hawatahama hadi serikali iwaonyeshe mahala sahihi pa kuhamia.
Awali Katika Tawala wa wilaya Kigoma,Mganwa Nzota Akitoa taarifa kwa Mkuu wa wilaya Kigoma, Rashid Chuachua aliyefika shule ya Msingi Majengo walipojihifadhiwa waathirika hao alisema kuwa jumla ya kaya 36 zimekumbwa na kadhia ya mvua hiyo kutoka maeneo hayo ya Katubuka na kwamba kaya sita zenye watu 47 ndizo zilizohamia shuleni hapo kuomba hifadhi huku watu wengine wakiomba hifadhi kwa ndugu na majirani.
pamoja na hilo Katibu Tawala huyo wa wilaya alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji na wadau wa maendeleo wametoa msaada wa magodoro kwa waathirika hao sambamba na chakula wakati taratibu nyingine za kuangalia changamoto hizo zikiendelea.
Akizungumza na waathirika hao Mkuu wa wilaya Kigoma,Rashid Chuachua alisema kuwa serikali imetoa hifadhi ya muda kwa waathirika hao lakini amewataka kuondoka shuleni hapo ili kutafuta maeneo mengine ya kujihifadhi kuwezesha shule hiyo kuendelea kutoa huduma kwa wanafunzi.
Mkuu huyo wa wilaya akizungumzia changamoto ya kujaa maji katika eneo hilo la Katubuka tangu mwaka 2023 na kuathiri nyumba ambazo wakazi wake wamehama alisema kuwa serikali ya wilaya na halmshauri wamenza tathmini kupitia mradi wa uboreshaji wa miji Tanzania (TACTIC) ili kuona namna ya kuwasaidia wakazi hao.
Sambamba na hao alisema kuwa pia wanashirikiana na Baraza la Taifa la uhifadhi wa mazingira (NEMC) na taasisi nyingine za serikali na wadau wa maendeleo katika kuwasiaidia waathirika hao ambapo wameshalifanyia tathmini eneo hilo hivyo wanaendelea na mchakato wa bajeti kuona hatua za kuchukua.
0 Comments