Na Amon Mtega,_Songea.
MKURUNGENZI msaidizi wa kituo cha kulelea watoto waliyotokea mazingira hatalishi(Yatima)cha Songea Women and Children Care Organization (SWACCO) Mkoani Ruvuma Anna Mugenya amemshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutoa msaada wa mahitaji ya chakula kwenye kituo hicho na kuwafanya watoto hao wafurahie sikukuu ya Eid Al-Adha ambayo ni ya kuchinja.
Mugenya ametoa shukurani hizo mbele ya mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ambaye alikabidhi mahitaji hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambayo yametolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Mugenya akipokea mahitaji hayo ambayo ni Mbuzi wawili Mchele ,Maharage,Sukari,Unga wa Ngano pamoja na mafuta ya kula amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wake Kassim Majaliwa imekuwa ikijali makundi mbalimbali yakiwemo ya watoto wanaotokea kwenye mazingira hatalishi.
"Tunamshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa msaada huo pamoja na Serikali ya Mkoa wa Ruvuma ambayo mara zote imekuwa begakwabega kuwa karibu na kituo hicho kwa kutatua changamoto zake"amesema Anna Mugenya.
Aidha Mugenya amesema kuwa kituo hicho kwa sasa chenye watoto 43 kimeshafanikisha kuwalea watoto hao na baadhi yao wamesomeshwa wapo kwenye vyuo na wengine wameajiliwa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya Elimu,Afya na Ulinzi .
Hata hivyo mtoto Boniface Komba anayesoma kidato cha tatu amesema kuwa misaada hiyo imewapa faraja na kujiona kuwa wapo sawa na watoto wengine ambao wapo na wazazi wao.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ambaye alikabidhi mahitaji hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameamua kushiriki sikuku ya Eid Mubarak kwa kutoa mahitaji kwenye kituo hicho cha kulelea watoto hao.
Mgema akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amesema kuwa kuna kila sababu ya kila mmoja au taasisi kuona umuhimu wa kuwajali watoto kwa kuwapelekea mahitaji mbalimbali ya kibinadamu ili kuwafanya watoto hao waendelea kuwa kwenye hali nzuri.
0 Comments