Header Ads Widget

WAZIRI WA ULINZI NA JKT ATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA UWANJA WA KIMATAIFA WA GOFU WA JWTZ DODOMA

 


Na Matukio Daima Media Dodoma 

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb.) tarehe 15 Julai, 2026 ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Uwanja wa Kimataifa wa Gofu unaotekelezwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika eneo la Ihumwa, jijini Dodoma, maarufu kama TPDF Golf Club.

Mara baada ya kuwasili katika eneo la mradi, Waziri alipokelewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, ambaye alimweleza kuwa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaendelea vizuri baada ya changamoto za upatikanaji wa fedha kupatiwa ufumbuzi.

 Amebainisha kuwa hatua hiyo imewezesha kasi ya ujenzi kuongezeka na shughuli za mradi kuendelea kama ilivyopangwa.

Akizungumza na maafisa na askari wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo, Dkt. Nyansaho amesema lengo la ziara yake ni kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo muhimu wenye matarajio makubwa ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla kupitia sekta ya utalii, michezo na diplomasia ya michezo.



Waziri huyo ameipongeza Kamati ya Ujenzi kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuzingatia viwango vya ubora katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo. Alieleza kuwa JWTZ imejijengea sifa ya kusimamia na kutekeleza miradi yenye ubora wa hali ya juu, hivyo ni muhimu kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.


Mradi huo unatarajiwa kukamilika katika miezi michache ijayo na utahusisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wenye mashimo 18 ya mchezo wa gofu, hoteli ya hadhi ya nyota tano, pamoja na miundombinu mbalimbali ya michezo na burudani ikiwemo mabwawa ya kuogelea, bustani ya wanyama (Zoo) na maeneo mengine ya mapumziko.

Baada ya kukamilika, Uwanja wa Kimataifa wa Gofu wa JWTZ utakuwa miongoni mwa viwanja vikubwa na vya kisasa zaidi nchini. 


Aidha, pamoja na TPDF Lugalo Golf Club, mradi huo utaifanya JWTZ kuwa taasisi ya kipekee nchini inayomiliki na kuendesha viwanja vya kisasa vya mchezo wa gofu vinavyokidhi viwango vya kimataifa.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI