Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Serikali kupitia Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia,wanawake na makundi maalum inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya kulelea wazee nchini ili kuwawezesha kuishi katika mazingira bora na kuimarisha ustawi wa maisha yao.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhandisi MaryPrisca Mahundi alisema hayo Julai 14 mkoani Kigoma alipofanya ziara kutembelea kituo cha kulelea wazee Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji Maarufu SILABU ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na wazee wanaotunzwa kwenye kituo hicho.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa serikali inajali mchango wa wazee wao kwa Taifa kwa muda wote na ndiyo maana serikali inachukua hatua kuhakikisha wazee hao wanatunza na kulindwa sambamba na kupatiwa bima hizo ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu yao.
Awali akisoma taarifa kwa Naibu Waziri Afisa ustawi wa jamii Mfawidhi wa kituo cha Makazi ya wazee Kibirizi SILABU Manispaa ya Kigoma Ujiji, Binura Abbas ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha makazi ya wazee na kuwezesha kupatikana kwa huduma muhimu ikiwemo malazi, chakula, mavazi na matibabu akiwashukuru wadau mbalimbali kwa kuunga mkono serikali kusaidia kituo hicho.
Pamoja na hilo Afisa Ustawi huyo wa kituo cha kulelea wazee alisema kuwa kituo hicho pia kinakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa majengo ya kituo pamoja na ukosefu wa uzio hivyo kupelekea usalama wa watu na mali za kituo hicho kuwa hatarini.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya Kigoma, Dk.Rashid Chuachua alisema kuwa serikali kupitia halmshauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji inasimamia kwa karibu utoaji huduma za kibinadamu kwa kituo hicho kupitia bajeti za serikali sambamba na kukutana na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakisaidia kuongeza nguvu katika kutoa huduma za kibinadamu.










0 Comments