Header Ads Widget

KAMISHNA MPYA TANAPA AAPISHWA ,KIJAJI ATAKA MAGEUZI

 

Na Pamela Mollel,Arusha 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amemtaka Kamishna mpya wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Gibril Mwishawa, kuimarisha utendaji wa shirika hilo kwa kuhakikisha sekta ya uhifadhi na utalii inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa


Akizungumza jijini Arusha wakati wa hafla ya kumuapisha Kamishna huyo, Waziri Kijaji anasema uongozi mpya unapaswa kuelekeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya hifadhi, kuongeza fursa za uwekezaji, kuanzisha bidhaa mpya za utalii na kusimamia mapato kwa ufanisi ili kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi wa nchi


 Pia alisisitiza umuhimu wa kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi, akieleza kuwa ushirikiano wao ni nguzo muhimu katika kulinda rasilimali za taifa

Aidha, alimwelekeza Kamishna kuhakikisha nidhamu, uadilifu, weledi na ustawi wa watumishi wa TANAPA vinaendelea kupewa kipaumbele

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara, anasema bodi itaendelea kushirikiana na menejimenti ya shirika hilo kwa kutoa ushauri na miongozo itakayosaidia kufanikisha malengo ya uhifadhi na maendeleo ya utalii nchini


Aliongeza kuwa uwazi katika uendeshaji wa shughuli za shirika pamoja na utoaji wa mrejesho kwa watumishi wa ngazi mbalimbali ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa

Naye Kamishna wa Uhifadhi, Massana Gibril Mwishawa, anasema ataiongoza TANAPA kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uzalendo, uadilifu na weledi, huku akisisitiza kuwa hifadhi za taifa zina nafasi muhimu katika kulinda bioanuwai, kuchochea uchumi na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mapato yatokanayo na utalii



Aliongeza kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kushika nafasi hiyo, akiahidi kushirikiana kwa karibu na watumishi wote wa TANAPA ili kuendelea kuimarisha mafanikio ya taasisi hiyo

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa taasisi mbalimbali za uhifadhi, akiwemo NCAA, TFS na TAWA, pamoja na viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya uhifadhi na utalii, viongozi wa dini, maafisa na askari wa TANAPA.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI