Header Ads Widget

UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA WAANZA SEPTEMBA, SERIKALI YASEMA UWAJIBIKAJI UMEIMARIKA

 

Na Matukio DaimaMedia 

Serikali imesema itaanza ukaguzi wa vyama vya ushirika nchini kuanzia Septemba mwaka huu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwajibikaji, kuongeza imani ya wanachama na kuboresha utendaji wa sekta hiyo inayochangia zaidi ya Dola za Marekani bilioni mbili katika uchumi wa taifa.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi wa Shirika la Wakaguzi na Wasimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Jeremia Jackson Mugeta, alisema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha vyama vyote vya ushirika vinakaguliwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria.


Alisema vyama vya ushirika vinapaswa kuandaa na kuwasilisha taarifa zao za fedha kwa ofisi za shirika katika mikoa yote ya Tanzania Bara ili kurahisisha utekelezaji wa mpango wa ukaguzi wa mwaka wa fedha 2025/26.


"Tunataka wanachama wa vyama vya ushirika waendelee kuwa na imani na vyama vyao kwa kuhakikisha fedha zinatumika kwa uwazi na taarifa za ukaguzi zinapatikana kwa wakati," alisema.


Mugeta alisema hali ya usimamizi wa vyama vya ushirika imeendelea kuimarika, akibainisha kuwa idadi ya vyama vinavyopata hati safi za ukaguzi imeongezeka kutoka asilimia nne katika miaka ya nyuma hadi kufikia asilimia 16 kwa 

Sasa


Aidha, alisema vyama vinavyopata hati zenye mashaka vimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka takribani asilimia 37 hadi asilimia tano, jambo alilosema linaonyesha kuongezeka kwa uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria za fedha.


Kwa mujibu wa Ngeta, pamoja na kufanya ukaguzi, taasisi hiyo inaendelea kutoa ushauri kwa viongozi wa vyama vya ushirika kuhusu usimamizi wa fedha, uandaaji wa taarifa za kifedha na uzingatiaji wa sheria na kanuni ili kuimarisha utendaji wa vyama hivyo.


Akizungumzia mchango wa sekta ya kilimo, alisema inaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania kwa kuchangia zaidi ya asilimia 26 ya Pato la Taifa, huku mazao yanayouzwa kupitia vyama vya ushirika yakichangia zaidi ya Dola za Marekani bilioni mbili.


Alisema Serikali itaendelea kuimarisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo ili kuongeza ufanisi wa sekta ya ushirika na kuwahakikishia wakulima huduma bora zitakazoongeza tija na kipato chao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI