Header Ads Widget

IFCU YAPAISHA UCHUMI WA MKOA WA IRINGA KUPITIA ZAO LA UFUTA WAUZA UFUTA KWA TSH BILIONI 5.53

 


NA MATUKIO DAIMA MEDIA

IRINGA.

Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima Mkoa wa Iringa (IFCU) kimesema mkakati wake wa kuendeleza zao la ufuta umeanza kuzaa matunda baada ya uzalishaji na mapato ya wakulima kuongezeka kwa kiwango kikubwa, huku malipo yaliyokwenda kwa wakulima yakiongezeka kutoka zaidi ya Sh bilioni 2.169 katika msimu uliopita hadi zaidi ya Sh bilioni 5.53 katika msimu wa 2025/2026.

Akizungumza katika mahojiano na Matukio Daima Media katika kipindi cha Tanzania ya leo, Meneja wa IFCU, Tumaini Lupola alisema chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1993 kimejikita katika kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo bora, elimu ya kilimo na masoko ya uhakika ili kuongeza uzalishaji na kipato cha wanachama wake.


Alisema baada ya kufanya utafiti katika wilaya za Iringa na Kilolo, IFCU iligundua kuwa zao la ufuta lilikuwa likilimwa kwa kiwango kidogo licha ya kuwa na fursa kubwa kiuchumi. Aidha, takwimu za uzalishaji wake hazikuwa zikifahamika na wakulima wengi walikuwa wakitegemea madalali waliowanunulia mazao kwa bei ndogo, jambo lililosababisha wengi kukata tamaa na kuacha kulima zao hilo.


Kutokana na hali hiyo, IFCU kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Iringa na halmashauri zake ilianza mkakati wa kuhamasisha uzalishaji wa ufuta kupitia usambazaji wa mbegu bora, utoaji wa elimu kwa wakulima na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Lupola alisema katika msimu uliopita IFCU ilisambaza tani 1.5 za mbegu bora za ufuta kwa wakulima, huku halmashauri nazo zikichangia upatikanaji wa mbegu hizo, alisema matumizi ya mbegu bora yameongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa, ambapo baadhi ya wakulima wamevunja rekodi za mavuno ikilinganishwa na mbegu walizokuwa wakitumia hapo awali.


Kwa mujibu wa Lupola, matokeo ya uwekezaji huo yameonekana wazi, alisema katika msimu uliopita IFCU ilikusanya kilo 860,207 za ufuta zilizowapatia wakulima zaidi ya Sh bilioni 2.169, lakini msimu wa 2025/2026 uzalishaji umeongezeka na kufikia zaidi ya kilo milioni 2.377, huku fedha zilizolipwa kwa wakulima zikifikia zaidi ya Sh bilioni 5.056.

           Mwenyekiti wa bodi ya IFCU 

Alisema ongezeko hilo la zaidi ya mara mbili ya uzalishaji limechochea uchumi wa maeneo mengi ya vijijini, hususan katika ukanda wa Isimani na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kilolo ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakikabiliwa na ukame na kutegemea misaada ya chakula.


"Katika msimu ambao mahindi na mpunga havikufanya vizuri kutokana na ukosefu wa mvua, wakulima waliolima ufuta waliweza kuuza mazao yao, kununua chakula, kusomesha watoto, kugharamia matibabu na hata kujenga nyumba," alisema Lupola.


Alibainisha kuwa gharama za uzalishaji wa ufuta ni ndogo ukilinganishwa na mahindi,alisema ekari moja ya mahindi huhitaji takribani kilo 10 za mbegu, wakati ufuta huhitaji kilo mbili pekee. Aidha, ufuta huhitaji matunzo machache na hustahimili ukame, jambo linaloufanya kuwa zao linalofaa katika mazingira ya mabadiliko ya tabianchi.


Akizungumzia bei za mazao, Lupola alisema kwa sasa gunia la mahindi huuzwa kwa wastani wa Sh40,000, wakati mara nyingi gunia hilo huzidi kilo 100 na kufikia kilo 140, hivyo kumfanya mkulima kupata chini ya Sh300 kwa kilo moja. Kwa upande wa ufuta, alisema kilo moja huuzwa kwa wastani wa Sh2,450, kiwango kinachoufanya kuwa miongoni mwa mazao yenye faida kubwa kwa wakulima.


Alisema mafanikio hayo yamechangiwa pia na matumizi ya mfumo wa Stakabadhi za Ghala na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ambapo wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi hushindana kununua mazao kupitia mfumo wa kielektroniki. Mfumo huo umeondoa utegemezi wa madalali na kuongeza ushindani wa bei kwa manufaa ya wakulima.


“kabla ya mazao kuuzwa, hukaguliwa katika maghala yenye leseni ili kuhakikisha yanakidhi viwango vinavyokubalika kimataifa. Baada ya hapo taarifa huwekwa kwenye mfumo wa TMX na kuwafikia wanunuzi waliosajiliwa, ambao huwasilisha zabuni zao bila kulazimika kufika eneo la mnada”alisema


Pamoja na mafanikio hayo, alisema changamoto kubwa iliyopo bado ni upatikanaji wa mbegu bora. Alieleza kuwa mbegu nyingi zinazotumiwa na wakulima wa Iringa ni za zamani na hutoa ufuta usio na ubora unaohitajika katika soko la kimataifa, tofauti na mbegu mpya zinazotumiwa katika baadhi ya mikoa kama Mtwara na Songwe.

Kutokana na hali hiyo, IFCU imeanza kuwawezesha wakulima kuzalisha mbegu bora za QDS na imekuwa ikiandaa ziara za mafunzo kwa wakulima katika mikoa inayofanya vizuri kwenye uzalishaji wa ufuta. Mwaka uliopita zaidi ya wakulima 25 walitembelea Mkoa wa Mtwara kujifunza teknolojia za uzalishaji na mfumo wa masoko, huku mpango ukiwa ni kupanua mafunzo hayo hadi Songwe na baadaye katika baadhi ya nchi zinazofanya vizuri kwenye uzalishaji na uchakataji wa ufuta.


Mbali na ufuta, IFCU imeanza kuhamasisha wakulima kuzalisha mazao mengine yanayostahimili ukame kama dengu na mbaazi ili kuongeza vyanzo vya mapato kwa wakulima katika vipindi tofauti vya mwaka na kupunguza utegemezi wa zao moja.


Aidha, chama hicho kimeanza kuwekeza katika miundombinu ya biashara kwa kununua magari ya kusafirisha mazao kutoka vijijini kwenda kwenye maghala ya biashara, alisema IFCU inalenga kuongeza idadi ya magari kila mwaka ili kupunguza gharama za usafirishaji na kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Alisisitiza kuwa lengo la IFCU si kuwafanya wakulima waache kulima mahindi, bali kuwahamasisha kutenga sehemu ya mashamba yao kwa mazao ya biashara yenye tija kubwa, alisema hatua hiyo itawasaidia wakulima kuwa na uhakika wa kipato hata pale mazao ya chakula yatakapokumbwa na changamoto za hali ya hewa au kushuka kwa bei sokoni.


Lupola alisema iwapo uzalishaji wa ufuta utaendelea kuongezeka, Mkoa wa Iringa utakuwa na uwezo wa kuvutia wawekezaji wa viwanda vya kuchakata zao hilo, hatua itakayoongeza thamani ya mazao, ajira na mapato ya wakulima pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.


Hata hivyo serikali imeweka mkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani wa zao kupitia Dira ya Maendeleo 2050 inalenga kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa, yenye tija na inayochangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa Tanzania. 


Katika zao la ufuta, mkazo utawekwa kwenye matumizi ya mbegu bora, kilimo cha kisasa, umwagiliaji, na udhibiti wa magonjwa na wadudu.


 Pia, kutakuwa na uongezaji thamani kupitia usindikaji wa ufuta ili kuongeza mapato ya wakulima na mauzo ya nje. Serikali na sekta binafsi zitashirikiana kuboresha masoko, miundombinu na upatikanaji wa pembejeo. 

Hatua hizi zitasaidia kuongeza uzalishaji wa ufuta, kuboresha kipato cha wakulima na kuimarisha maendeleo ya taifa kwa ujumla.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI