Na Matukio Daima Media
Dar es Salaam.
Wasanii, wanamichezo, waandishi wa habari, viongozi wa dini na wananchi kutoka makundi mbalimbali wanatarajiwa kukutana kesho katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kwenye Dua Maalum ya kuwaombea na kuwaenzi waliotangulia mbele ya haki.
Mratibu wa dua hiyo, msanii Steve Nyerere, amesema lengo la tukio hilo si kuwaombea marehemu pekee, bali pia kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa hayo ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 31, 2026, Steve amesema dua hiyo itaanza saa 12:00 asubuhi na itaongozwa na masheikh pamoja na wachungaji, huku ikiwakutanisha watu wa kada mbalimbali bila kujali tofauti zao.
"Kesho tutawakumbuka wote waliotangulia mbele ya haki, wakiwemo wasanii, wanamichezo, waandishi wa habari na viongozi mbalimbali. Tunawaalika Watanzania wote tushirikiane kuwaombea na pia kuliombea Taifa letu," amesema.
Amesema amani ambayo Tanzania imeendelea kuwa nayo ni urithi unaopaswa kulindwa na kila Mtanzania, hivyo amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kudumisha upendo, uvumilivu na kuheshimiana.
"Tunataka kuendelea kuwa Taifa lenye umoja. Dua hii ni ya Watanzania wote na ni nafasi ya kutafakari mchango wa waliotutangulia pamoja na wajibu wetu wa kuendeleza amani waliyoiacha," amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Nyoshi El Saadat amesema tukio hilo lina umuhimu mkubwa kwa jamii na linapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote kwa kujitokeza kwa wingi.
Naye msanii Abdallah Mkumbila, maarufu Muhogo Mchungu, amesema kuwaombea waliotangulia mbele ya haki ni sehemu ya kuenzi mchango wao kwa jamii.
"Hatufahamu hali ya waliotutangulia huko waliko, lakini tunafahamu kuwa kuwaombea ni jambo jema na la muhimu kwa kila mmoja wetu," amesema.
Kwa upande wake, Ally Choki amesema siku hiyo itakuwa ya baraka kwa wote watakaoshiriki, huku akitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi.
Naye Andrew Sekidia amesema waliotangulia wameacha urithi wa amani na mshikamano ambao umeifanya Tanzania kuendelea kuwa mfano wa utulivu, hivyo kuna wajibu wa kuulinda kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania, Salum Abdul 'Chiky', amesema dua hiyo itawakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kuwaenzi wenzao waliotangulia mbele ya haki na kuimarisha mshikamano miongoni mwa Watanzania.
"Tunaamini dua ni jambo lenye baraka. Tunawaomba Watanzania wote wajitokeze kwa wingi tushirikiane kuwaombea wenzetu waliotangulia mbele ya haki na kuliombea Taifa letu," amesema.







0 Comments