Na Matukio Daima Media
Shirika la Kimataifa la watetezi wa haki za binaadamu, Defend Defenders limeipa Shirika la wanahabari ya kusaidia jamii za asili(MAIPAC) vifaa vya Ofisi ili kurahisisha utendaji kazi kwa kidigitari.
Vifaa hivyo, vipya vya kisasa vimekabidhiwa leo Julai 9,2026 MAIPAC na Kampuni ya uuzaji wa vifaa vya kidigitari ya Soud& Vision Ltd ya jijini Arusha,baada ya kulipiwa na shirika hilo la kimataifa.
Defend Defenders kabla ya kutoa msaada huo kwa MAIPAC ,lilifanya ukaguzi wa usalama wa TEHAMA kwa mashirika mbalimbali katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na hivyo, kubaini MAIPAC kuwa na uhitaji wa vifaa vya kisasa vya ofisi na MAIPAC kuomba msaada huo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma amesema, vifaa hivyo vitasaidia sana utendaji kazi wa MAIPAC na utunzwaji wa kanzi data kwa muda mrefu.
"Tunawashukuru sana Defend Defenders kwa msaada huu mkubwa, ambao sasa utawezesha MAIPAC kuboresha utendaji kazi na mfumo wa usalama kidigitari ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na wanachama wake"amesema
Amesema Defend Defenders ni shirika ambalo limekuwa na mahusiano kwa muda sasa na MAIPAC kwani tayari liliwahi kutoa mafunzo kwa wanahabari kuhusiana na masuala ya Kisaikolojia na ustawi kwa wanahabari na pia masuala ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na masuala ya utafutaji rasilimali kwa Asasi za kiraia.
"Defend Defenders wamekuwa wadau wetu wakubwa na tumekuwa na ushirikiano mzuri tangu, tulipounganishwa na Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu nchini(THRDC),kupitia mafunzo mbali mbali ya uboreshwaji utendaji kazi kwa watetezi wa haki za binaadamu"amesema
Juma alieleza kumshukuru sana Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Hassan Shire kwa misaada mbali mbali kwa MAIPAC na mashirika mengine na kuomba ushirikiano huo kuendelea kuimarishwa zaidi ili kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo watetezi wa haki za binaadamu.
Kwa upande wake, Meneja Utawala wa MAIPAC, Andrea Ngobole alisema,msaada huo pia utasaidia utunzwaji mzuri wakumbukumbu za wanachama wake ambao ni wanahabari na hivyo, kuwezesha kupatiwa mafunzo mara kwa mara kulingana na mahitaji.
Awali,Msimamizi wa mifumo ya TEHAMA wa Defend Defenders Hillary Kahoza alipotembelea MAIPAC alishauri uboreshwaji wa mifumo wa TEHAMA ili kuhifadhi vyema taarifa na kujilinda na wadukuzi mitandaoni.
Hata hivyo, Kahoza alipongeza shirika la MAIPAC kwa kazi nzuri linazofanya hasa katika kutoa elimu kwa wanahabari na wananchi ya jamii za asili kuhusiana na matumizi sahihi ya mitandao na masuala ya usalama katika mitandao na uzingatiaji wa sheria katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Shirika MAIPAC limekuwa na miradi kadhaa ikiwepo mradi wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maarifa ya asili mradi uliofadhiliwa na shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) kupitia programu ya miradi midogo ya mfuko wa mazingira duniani(GEF) na Ofisi ya makamu wa Rais(mazingira), Mradi wa kupinga ukeketaji wilayani Longido,Mradi wa utunzaji vyuanzo vya maji kijiji cha Selela wilaya ya Monduli mradi wa ujuzi wa kidigitari kwa wanafunzi wa kike.
Kwa wanahabari MAIPAC imekuwa na mradi wa kufundisha wanahabari uandishi wa habari za amani,mradi kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, ,mradi wa kuwafundisha wanahabari 140 nchi nzima uandishi wa mazingira na sheria zake, unofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni(UNESCO)
MAIPAC pia limekuwa shirika la kwanza nchini, kuandaa Kitabu juu ya umuhimu wa maarifa ya asili katika utunzwaji wa mazingira,kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzwaji wa vyanzo vya maji,kitabu ambacho kimesambazwa bure kwa lengo ya kushawishi maarifa ya asili ambayo kila jamii inayo yaunganishwe na maarifa ya kisasa na kutumiwa na watungaji ya sera kwa manufaa ya taifa.
MWISHO.








0 Comments