Na Matukio DaimaMedia
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, amesema uamuzi wa benki hiyo kuendelea na kiwango cha riba ya sera cha asilimia 6.25 unalenga kudhibiti mfumuko wa bei, kuhakikisha benki zinaendelea kuwa na ukwasi wa kutosha kutoa mikopo na kuimarisha utulivu wa uchumi nchini.
Akizungumza alipotembelea banda la BOT katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Tutuba alisema kiwango hicho kilifikiwa baada ya tathmini ya hali ya uchumi wa ndani na mwenendo wa uchumi wa dunia.
Alisema BOT inaendelea kulenga kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya kiwango cha asilimia tatu hadi tano, huku ukwasi ukiendelea kuwepo katika mfumo wa benki ili kuwezesha ukuaji wa mikopo na shughuli za kiuchumi.
"Tunaamini kiwango hiki kitaendelea kuleta utulivu wa bei na kuhakikisha fedha zinapatikana kwa kiwango kinachohitajika kuendesha shughuli za uchumi," alisema.
Tutuba alisema kipindi cha mavuno kinachokaribia kinatarajiwa kuongeza mzunguko wa fedha na kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania, hatua ambayo itawasaidia wakulima na wafanyabiashara kupata thamani stahiki ya mazao yao.
Mbali na sera ya fedha, alisema BOT inaendelea kukamilisha maandalizi ya sheria na kanuni za kusimamia mali za kidijitali (virtual assets), zikiwemo sarafu za kidijitali, ili kulinda watumiaji wa huduma hizo na kuzuia matumizi yake katika utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
Pia alisema mfumo wa Sema na BOT umeongeza ufanisi katika kupokea na kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha, huku juhudi zikiendelea kupanua wigo wa mfumo huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Akizungumzia maadhimisho ya miaka 60 ya BOT, Tutuba alisema taasisi hiyo imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha, mifumo ya malipo na utulivu wa uchumi, hali iliyochangia kuongeza imani ya wawekezaji na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa na uchumi imara licha ya changamoto za kimataifa.







0 Comments