Fadhil Abdallah,Kigoma
Waziri wa uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameitaka kampuni ya meli nchini (TASHICO) kusimamia kwa karibu ukarabati mkubwa unaofanywa kwa meli ya Mv.Liemba na kuhakikisha meli hiyo inafanya kazi kufikia mwisho wa mwezi Julai mwaka huu.
Waziri Mbarawa alisema hayo alipofanya ziara katika bandari ya Kigoma kuangalia maboresho ya miundo mbinu katika bandari hiyo na ukarabati wa meli hiyo ambapo alisema kuwa wananchi wanaoishi mikoa ya Kigoma,Rukwa na Katavi wanaitaka meli ya Mv.Liemba kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi na maisha yao hivyo amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha mwisho wa mwezi Julai meli hiyo inaanza kufanya kazi.
Alisema kuwa ameongea na wahandisi na wasimamizi wa mradi huo waliomueleza ukarabati umefikia asilimia 90 hivyo ukarabati huo utakamilika kufikia Julai 15 mwaka huu ambapo alisema kuwa wasimamizi wa mradi huo wameeleza kuwa hakuna changamoto zozote zitakazozuia mpango huo na kwamba wamemuhakikishia kwamba mradi huo wa ukarabati meli ya Mv.Liemba utakamilika kama walivyotoa taarifa.
“kwetu sisi meli hii ni muhimu kwa maisha ya wananchi wanaoishi mwambao wa ziwa Tanganyika kwani imekuwa mkombozi na kichocheo kwa shughuli za kiuchumi na maisha yao, tunaitaka sana meli hii ifanye kazi kwani itatekeleza kwa vitendo mpango wa serikali wa kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa mkoa wa kimkakati kwa shughuli za uchumi na biashara,”Alisema Waziri huyo wa uchukuzi.
Awali meneja wa mradi wa ukarabati wa meli ya Mv.Liemba, Mhandisi Elius Kivara alisema kuwa ukarabati wa meli hiyo utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 33 na kwamba hadi sasa ukarabati huo umefikia asilimia 90 na kwamba kufikia julai 15 mwaka huu wataanza kufanya majaribio ya meli hiyo baada ya kufungwa kwa injini na vifaa vipya kwenye maeneo mbalimbali ya meli hiyo,
Mwisho.









0 Comments