Chadema ni kiwanda cha kutengeneza chuki – UVCCM.
-Yataka watanzania wasiwe wateja wa bidhaa zake.
Na Mwandishi Wetu, Mbozi.
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Songwe umekituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kueneza chuki na upotoshaji kupitia mikutano ya Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, iliyofanyika hivi karibuni mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 26, 1026 katika Ofisi za CCM Mkoa wa Songwe zilizopo Vwawa, Wilaya ya Mbozi, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Songwe, Fatuma Husein, amedai CHADEMA kimegeuka kuwa "kiwanda cha kutengeneza chuki" na kuwataka Watanzania kutokubali kuwa wateja wa bidhaa zinazotoka kwenye kiwanda hicho.
Fatuma amesema lengo la CHADEMA ni kuwagawa Watanzania badala ya kuimarisha amani na mshikamano, akiwataka wananchi kupuuza kauli anazodai zinachochea migawanyiko na kuendelea kulinda umoja wa taifa.
Aidha, amewatuhumu baadhi ya viongozi wa CHADEMA kueneza taarifa za uongo na upotoshaji kwa maslahi ya kisiasa, akisisitiza wananchi wanapaswa kuwa makini na kauli zinazolenga kupotosha umma.
Akizungumzia hoja ya Katiba Mpya, Fatuma amesema Ilani ya CCM imeahidi kuendeleza mchakato huo na kudai kuwa wapo wanaoweza kujaribu kuuvuruga endapo utaanza, huku akiwataka vijana kuendelea kuombea amani na utulivu wa nchi.
Kuhusu madai ya upendeleo yaliyotolewa kwenye mikutano hiyo katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, amekanusha kuwepo kwa ubaguzi wa kisiasa, akieleza kuwa hakuna muombaji anayehitajika kuonyesha kadi ya chama ili kupata mkopo huo.
Amesema Mkoa wa Songwe umetoa zaidi ya Sh bilioni tatu za mikopo katika mwezi Juni pekee, huku Serikali ikiendelea kuwawezesha vijana kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Soko la Madini Songwe, Soko la Wamachinga Tunduma, Soko la mazao Momba na mafunzo ya ufundi kupitia VETA, DIT, na Chuo cha Vijana Sasanda.
Fatuma ameongeza kuwa miradi ya helium Momba na Ngwala, uchimbaji wa makaa ya mawe Ileje pamoja na ujenzi wa maghala na machinjio ya kisasa imeongeza fursa za ajira kwa vijana, akisisitiza kuwa Serikali hutoa mikopo bila ubaguzi wa kisiasa na kuwataka wanufaika kurejesha mikopo kwa wakati badala ya kuigeuza hoja hiyo kuwa ajenda ya kisiasa.
Mwisho.





0 Comments