Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ametoa rai kwa watoa huduma za Utalii na Uhifadhi nchini kuzingatia ubora wa huduma za viwango vya kimataifa kwa watalii wanaokuja nchini sambamba na kuzingatia misingi na miiko ya kazi, wakiongozwa na uzalendo kwa nchi.
Waziri Kijaji amesemwa leo Juni 19, 2026 Jijini Arusha alipokuwa akifunga mafunzo kwa madereva wa utalii wapatao 100 yaliyofadhiliwa na kampuni ya Superdoll.
Dkt. Kijaji amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa programu maalumu iliyoasisiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuwajengea uwezo waongoza watalii na wadau wengine wa utalii.
"Leo hii tunashuhudia waongoza watalii zaidi ya 100 pamoja na wale madereva 10 kutoka TANAPA mnahitimisha mafunzo yenu. Siku chache zilizopita waongoza watalii wapatao 2000 walipatiwa mafunzo kama haya hapa Jijini, Arusha. Elimu mliyoipata leo ni uwekezaji kwa taifa. Tunatarajia kuona matokeo yake kupitia huduma bora zaidi, mawasiliano bora, usalama zaidi na uzoefu kwa watalii wanaotembelea Tanzania” Alisema Dkt.Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji amesisitiza kutoa huduma kwa weledi, ukarimu na moyo wa dhati kwa wageni wanaokuja nchini ili kuwapa kumbukumbu nzuri isiyosahaulika.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Superdoll Bw. Seif Seif amesema kinachofanywa na kampuni hiyo ni kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika sekta ya utalii ili madereva hao waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Awali, akitoa salamu za Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Jacob Rombo amesema mafunzo yaliyofadhiliwa na kutolewa na kampuni ya Superdoll yametolewa kwa wakati sahihi na yanakwenda kuongeza thamani na ubora wa huduma za utalii hususani wakati Jiji la Arusha likijiandaa kupokea mashindano ya AFCON 2027 pamoja ugeni wa Maspika wa Umoja wa Mabunge duniani hapo mwezi Oktoba mwaka huu.














0 Comments