Katika ziara hiyo, Mhe. Balozi Yakubu alitembelea vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi, pamoja na kiwanja cha gofu cha “The General Waitara Serengeti Golf Course”, eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Serengeti, pamoja na eneo la Nyatwali, maarufu kama Speke Gulf ambapo Serikali inaendelea na taratibu za kuwalipa wananchi fidia ili kupisha shughuli za uhifadhi, kwa kuwa eneo hilo ni sehemu ya ushoroba muhimu unaotumiwa na wanyamapori kupita kutoka eneo moja kwenda jingine.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Balozi Yakubu alisema ujenzi wa uwanja wa ndege utasaidia kuugeuza mji wa Serengeti kuwa kitovu cha utalii, kwa kurahisisha ufikaji wa mamia ya watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na hivyo kuongeza fursa za utalii pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Serengeti ni hazina ya asili ya Tanzania na mojawapo ya mifumo muhimu zaidi ya ikolojia ya wanyamapori duniani, ikiwa na bioanuwai kubwa na uhamaji wa nyumbu unaotambulika kimataifa. Uwekezaji katika miundombinu ya usafiri unaendelea kuwa sehemu muhimu ya kufungua zaidi fursa za utalii na maendeleo nchini.













0 Comments