Header Ads Widget

UCSAF YALENGA KUCHOCHEA UCHUMI WA KIDIJITALI VIJIJINI



NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeeleza kuwa upanuzi na uboreshaji wa huduma za mawasiliano Nchini unalenga kuwawezesha wananchi, hususani waliopo maeneo ya vijijini, kutumia intaneti katika shughuli za kiuchumi na kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Akizungumza katika mafunzo ya wahariri Mkoani Mwanza Mkuu wa Kanda ya Ziwa UCSAF, Fredy Kandonga, amesema uwekezaji unaofanywa kupitia mfuko huo siyo tu kuongeza upatikanaji wa mtandao wa simu, bali pia kujenga mazingira yatakayowawezesha wananchi kutumia teknolojia katika biashara, huduma za fedha, elimu, afya na upatikanaji wa taarifa.

Kandonga amesema hadi Aprili 2026, makubaliano yalifikiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika kata 2,293 zenye vijiji 5,505 na wakazi zaidi ya milioni 32.7, ambapo minara 2,324 imepangwa kujengwa kwa gharama ya Sh bilioni 29 na mradi unatarajiwa kukamilika Machi 2027.

Amesema katika Kanda ya Ziwa minara 67 inajengwa katika mikoa ya Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu, ambapo mnara mmoja tayari umewashwa na wananchi wameanza kupata huduma.

“Katika awamu hii ya 10, Mkoa wa Geita unajengwa minara saba, Kagera minara 14, Mara minara 11, Mwanza minara 21, Shinyanga minara sita na Simiyu minara nane,” amesema Kandonga.


Amesema sambamba na ujenzi wa minara mipya, UCSAF imeendelea kuboresha minara iliyopo ili kuongeza kasi na ubora wa intaneti kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Kandonga, minara 431 imeboreshwa kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G/4G, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuongeza uwezo wa wananchi kutumia huduma za kidijitali, huku Serikali ikitoa ruzuku ya Sh bilioni 9.14 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Amesema maboresho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kutumia huduma za elimu mtandao, afya mtandao, biashara mtandao pamoja na huduma za kifedha kupitia simu, hatua inayoweza kuongeza ufanisi wa shughuli zao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kandonga amesisitiza kuwa mawasiliano ni sehemu muhimu ya uchumi wa sasa, hivyo maeneo yasiyokuwa na huduma za uhakika za simu na intaneti yanaweza kukosa fursa zinazotokana na teknolojia.

“UCSAF itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya umma na binafsi kufikia Tanzania ya kidijitali. Tupo tayari kushirikiana na wadau wote, wakiwemo Wahariri wa Habari, kubaini na kutatua changamoto za mawasiliano nchini,” amesema"Alisema Kandonga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa UCSAF, Celina Mwakabwale, amesema ushirikiano na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanafahamu miradi inayotekelezwa na mfuko huo pamoja na namna inavyowanufaisha.

Amesema Wahariri wana nafasi muhimu katika kuratibu maudhui yanayowafikia wananchi, hivyo ushirikiano huo utasaidia kutoa taarifa sahihi kuhusu maeneo yanayofikiwa na huduma za mawasiliano na fursa zinazotokana na uwepo wa huduma hizo.


Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko, amewataka waandishi wa habari kutumia maarifa waliyoyapata kuelimisha jamii kuhusu shughuli za UCSAF, huku wakifuatilia changamoto za mawasiliano katika maeneo ya vijijini.

“Waandishi wa habari wawe daraja kati ya UCSAF na jamii, waelimishe jamii wafahamu mfuko huo ni nini, upatikanaji wa huduma zao ukoje na tuwatazame hasa wananchi wa maeneo ya vijijini,” amesema Soko.

Soko amesema uwepo wa huduma bora za mawasiliano katika maeneo ya vijijini unaweza kuwa kichocheo cha uchumi wa kidijitali kwa kuwa wananchi wataweza kutumia simu na intaneti kufanya biashara, kupata huduma za kifedha, elimu, taarifa za masoko pamoja na huduma nyingine muhimu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI