Timu ya wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili inashiriki katika kambi maalum ya upasuaji wa macho wa kibingwa na kibingwa bobezi inayofanyika katika Hospitali ya Kamuzu Central (KCH), jijini Lilongwe, Malawi. Ushiriki huo umefanyika kufuatia mwaliko maalum kutoka kwa Rais wa Vision Care, Dkt. Donghae Kim, ambapo timu ya Muhimbili imepata fursa ya kuungana na wataalamu wa Vision Care katika kutoa huduma za matibabu ya macho kwa wananchi wa Malawi.
Vision Care ni shirika la kimataifa lenye makao makuu nchini Korea Kusini, linalojikita katika kupambana na kupunguza tatizo la upofu duniani kupitia huduma za afya ya macho, matibabu na upasuaji. Kupitia ushiriki huo, wataalamu wa Muhimbili wamekuwa sehemu ya timu ya kimataifa inayoshirikiana katika kutoa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi kwa wagonjwa wenye changamoto mbalimbali za macho.
Ushiriki wa Muhimbili katika kambi hiyo unaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya, huku ukitoa fursa kwa wataalamu wa Tanzania kushirikiana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali katika kuboresha huduma za macho. Pia, kambi hiyo inaonesha nafasi ya Muhimbili katika kushiriki juhudi za kimataifa za kupunguza mzigo wa upofu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za macho kwa wakati.










0 Comments