Header Ads Widget

PROF SANGA; ELIMU MBADALA INAENDELEA KUTOA FURSA YA PILI KWA WALIOKOSA MASOMO

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

MKUU wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE), Profesa Philipo Sanga, amesema elimu nje ya mfumo rasmi imeendelea kuwa mkombozi kwa maelfu ya vijana na watu wazima wanaokosa fursa ya kuendelea na masomo kupitia mfumo wa kawaida wa elimu.

Akizungumza katika banda la taasisi hiyo wakati wa Wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea jijini Dodoma, Prof. Sanga amesema elimu mbadala imekuwa daraja muhimu la kuwafikia wananchi walioshindwa kuanza shule kwa wakati au waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali za maisha.

Amesema miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya watoto na vijana kushindwa kukamilisha masomo yao ni umaskini, mimba za utotoni, ndoa za mapema pamoja na mazingira mengine ya kijamii na kiuchumi.

“Tunatoa fursa kwa wananchi hawa kuendelea na masomo yao kupitia mifumo mbadala ya ujifunzaji ili waweze kupata maarifa, stadi na elimu inayowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” amesema Prof. Sanga.

Amesema taasisi hiyo inaendesha programu mbalimbali za elimu ya msingi na sekondari kwa njia mbadala, sambamba na mafunzo ya elimu ya juu yanayolenga kuandaa wataalamu wa elimu nje ya mfumo rasmi na maendeleo ya jamii.

Kwa mujibu wake, ongezeko la idadi ya wanaojiunga na programu za taasisi hiyo kila mwaka linaonesha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma za elimu mbadala nchini.

Prof. Sanga amesema IAE pia ina jukumu la kusajili na kusimamia shule huria ili kuhakikisha zinatoa elimu inayokidhi viwango vya ubora vilivyowekwa.

Aidha, ametoa wito kwa wadau wa elimu kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kujifunzia ikiwemo maabara, maktaba na vifaa vya TEHAMA ili kuongeza ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi wa mifumo mbadala.

Amesisitiza kuwa elimu nje ya mfumo rasmi ni sehemu muhimu ya jitihada za kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kujifunza na kufikia ndoto zake licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza katika safari ya elimu.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI