Header Ads Widget

DC VICTORIA MWANZIVA AMZAWADIA ‘IRON LADY’ ELLEN JOHNSON SIRLEAF KINYAGO CHA UJAMAA

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mkoa wa Lindi-Tanzania, Mhe. Victoria Mwanziva akimkabidhi zawadi ya kinyago cha Ujamaa, Rais wa kwanza mwanamke Barani Afrika, Rais Mstaafu wa Liberia, Mhe. Ellen Johnson Sirleaf.
 


MKUU wa Wilaya ya Lindi, Mkoa wa Lindi-Tanzania, Mhe. Victoria Mwanziva ambaye yupo nchini Liberia kwa mafunzo maalum ya Uongozi, amemzawadia zawadi ya kinyago cha Ujamaa, Rais wa kwanza mwanamke Barani Afrika, Rais Mstaafu wa Liberia, Mhe. Ellen Johnson Sirleaf.

Zawadi hiyo imetolewa kama ishara ya upendo, umoja na ukarimu wa Kitanzania.

Mhe. Victoria Mwanziva ni mshiriki wa Programu mahususi na maalumu ya Uongozi kwa Wanawake inayoratibiwa na Rais Mstaafu huyo, inayojulikana kama “Amujae Leadership Initiative” ipo chini ya Ellen Johnson Sirleaf Presidential Centre for Women and Development – EJS Centre.

Akizungumza baada ya kumkabidhi zawadi hiyo, DC Mwanziva alielezea maana ya Kinyago hicho kuwa ni alama ya Ujamaa – falsafa iliyojenga umoja wa Watanzania. Rais Mstaafu Sirleaf amefurahi na kueleza ataweka kinyago hicho kwenye Ofisi za EJS Liberia kama kumbukizi ya thamani.

“Kwangu ni heshima kubwa kukutana na kiongozi mahiri duniani kama Mama Ellen Johnson Sirleaf – Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika. 

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mkoa wa Lindi-Tanzania, Mhe. Victoria Mwanziva akiwa na zawadi ya kinyago cha Ujamaa, wakati wa tukio hilo la kumkabidhi Rais wa kwanza mwanamke Barani Afrika, Rais Mstaafu wa Liberia, Mhe. Ellen Johnson Sirleaf.
 


Pia nimemwambia Tanzania tuna mwanamke jasiri, shupavu na kipenzi cha Watanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anaendelea kuinua wanawake katika nyanja zote, ikiwemo uongozi,” amesema DC Mwanziva.

Mhe. Victoria Mwanziva, ni miongoni mwa Wanawake 15 Barani Afrika waliopata bahati ya kuchaguliwa kwenye program hiyo  maalum ya Uongozi kwa Wanawake, mafunzo ambayo yanafanyika nchini Liberia na Sierra Leone.

Baadhi ya Washiriki hao wengine kwenye program hiyo ni: Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii wa Namibia Mhe Dkt Esperance Luvindao, Waziri wa Mazingira wa Guinea Mhe Djami Diallo, Wabunge mbalimbali kama Mbunge kundi la wanawake kutoka Senegal Mhe Anta Diack na wanawake Viongozi wa Mashirika na Taasisi mbalimbali barani Afrika kama Dr. Anneline Chetty Mtendaji mkuu wa kituo cha Biashara, Viwanda na Uwekezaji Afrika ya Kusini.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI