Kampuni ya kuzalisha bidhaa za watoto na akina mama, Bumpietz, imetoa ufadhili wa mwaka mmoja kwa mama aliyejifungua mapacha watano, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha mshikamano na kusaidia familia zinazokabili changamoto za malezi ya watoto wachanga.Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, mwakilishi wa kampuni ya Bumpietz, Lwiza Fulgence, alisema kuwa kampuni hiyo imeguswa na tukio hilo la kipekee na kuamua kujitokeza kutoa msaada utakaomsaidia mama huyo katika kuwalea watoto wake.
Lwiza alisema kuwa kujifungua watoto watano kwa wakati mmoja ni jambo linalohitaji maandalizi makubwa na matumizi ya kila siku ya bidhaa mbalimbali za watoto, hali ambayo inaweza kuwa mzigo mkubwa kwa familia husika.
Kutokana na hali hiyo, Bumpietz imeona umuhimu wa kushiriki jukumu la kijamii kwa kutoa bidhaa muhimu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“Tumeguswa sana na tukio hili. Kama wazalishaji wa bidhaa za watoto na akina mama, tumeona ni muhimu kuwa sehemu ya furaha hii kwa kutoa msaada utakaowezesha watoto hawa kupata mahitaji muhimu katika hatua zao za mwanzo za maisha,” alisema Lwiza.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji, hususan watoto na akina mama, kwa kuwa wao ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii yoyote.
Kwa upande wake mnufaika aliyepokea msaada huo alieleza shukrani zake kwa kampuni ya Bumpietz kwa moyo wa kujitolea waliouonyesha.
Alisema msaada huo umempa matumaini makubwa kutokana na changamoto za kulea watoto watano wachanga kwa wakati mmoja.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo pia waliipongeza kampuni hiyo kwa hatua yake ya kuwajibika kijamii na kuwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia familia hiyo ili kuhakikisha watoto hao wanapata malezi bora na mahitaji yote muhimu.
Ufadhili huo unatarajiwa kujumuisha bidhaa mbalimbali za watoto zinazozalishwa na kampuni ya Bumpietz, jambo litakalosaidia kupunguza gharama za malezi kwa familia hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja.
Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa na wengi, huku ikitajwa kuwa mfano mzuri wa mshikamano na upendo kwa jamii.






0 Comments