Header Ads Widget

ZIARA YA RAIS DKT SAMIA URUSI NA UJUMBE WA TANZANIA SI KISIWA TENA

Na .Francis Godwin ,Matukio Daima Media

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya  ziara ya siku tatu nchini Urusi kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026, pamoja na  kufanya mazungumzo rasmi na Rais Vladimir Putin pamoja na kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026). 


Ziara hii imeibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya Tanzania katika diplomasia ya kimataifa na umuhimu wa kuendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali duniani.

Ziara hii ni ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya pili kwa Rais wa Tanzania kutembelea Urusi tangu mwaka 1969 alipofanya hivyo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere. 

Pia ni ziara ya kwanza ya Rais Samia nje ya Bara la Afrika tangu uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, jambo linaloonyesha dhamira ya serikali ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa Ikulu ya Tanzania, ziara hiyo ililenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi katika sekta mbalimbali za kimkakati zikiwemo biashara na uwekezaji, elimu, sayansi na teknolojia, nishati, madini, kilimo na miundombinu.

 Hizi ni sekta ambazo zina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.

Katika dunia ya sasa, hakuna taifa linaloweza kujiendesha kwa kujitenga na mataifa mengine. 

Tanzania nayo si kisiwa. Maendeleo ya uchumi, biashara, teknolojia na uwekezaji yanahitaji ushirikiano wa karibu na mataifa mbalimbali. 

Ndiyo maana ziara za viongozi wakuu wa nchi katika mataifa mengine zinaendelea kuwa sehemu muhimu ya diplomasia ya maendeleo.

Mwanadiplomasia wa mkoani Iringa, Luciana Mbosa, ameisifu ziara hiyo akieleza kuwa imekuja wakati mwafaka ambapo Rais Samia anaendelea kuunganisha Watanzania na kuitangaza nchi kimataifa.

 Kwa mujibu wake, ushiriki wa Tanzania katika majukwaa makubwa ya kiuchumi duniani unatoa nafasi ya kutangaza vivutio vya utalii, kuvutia wawekezaji na kufungua masoko mapya ya bidhaa za Tanzania.

Huku Marcelina Mkini mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake Tanzania (UWT)wilaya ya Mufindi  amepongeza uamuzi wa Rais Samia kutembelea Urusi, akisema kuwa ni hatua inayodhihirisha uwezo wa Tanzania kujenga mahusiano ya kirafiki na mataifa mbalimbali bila kujali tofauti za kisiasa zilizopo duniani.

 Anaamini kuwa ushirikiano huo unaweza kuleta manufaa katika elimu, teknolojia na uwekezaji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Omari Sanga ni mkazi wa Kilolo  amesema anatamani kuona ziara za aina hiyo zikiendelea kufanyika katika mataifa mengine makubwa duniani.

 Kuwa Tanzania inapaswa kuendelea kupanua wigo wa ushirikiano wake wa kimataifa ili kupata uzoefu, teknolojia na mitaji inayohitajika katika safari ya maendeleo.

Wapo wanaojiuliza kuhusu umuhimu wa ziara hiyo wakati Urusi inaendelea kukabiliwa na changamoto za vita vilivyochukua zaidi ya miaka minne na nusu.

 Hata hivyo, ukweli ni kwamba mataifa mengi duniani yanaendelea kushirikiana na Urusi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kidiplomasia. 

Ushiriki wa viongozi wa mataifa tofauti katika jukwaa la SPIEF unaonyesha kuwa Urusi bado ni mshiriki muhimu katika uchumi wa dunia hivyo uamuzi wa Rais Dkt Samia ni uamuzi wenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

Kwa Tanzania, jambo la msingi ni kuhakikisha maslahi ya taifa yanatangulizwa. 

Ziara ya Rais Samia nchini Urusi ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha diplomasia ya uchumi, kuvutia uwekezaji na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa. Ni ujumbe kwamba Tanzania si kisiwa; ni sehemu ya jamii ya kimataifa inayotafuta ushirikiano, maendeleo na ustawi wa wananchi wake.

Kwani kupitia ziara hiyo ya kihistoria inajipambanua kuwa Tanzania si kisiwa tena ni nchi yenye misingi bora ya Kidiplomasia .

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI