Na Matukio Daima Media
KIJANA mdau wa maendeleo wa Tarafa ya Kalenga, Fadhil William Mgeni, amechangia zaidi ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya kuunga mkono uanzishwaji wa Jukwaa la Wanawake Kiuchumi, Maendeleo na Siasa katika Tarafa ya Kalenga, Wilaya ya Iringa.
Mchango huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha na kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo na uongozi ndani ya jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo uliofanyika leo katika Kijiji cha Kalenga, Fadhil alisema amevutiwa na kazi kubwa inayofanywa na Diwani wa Kata ya Kalenga, Shakira Kiwanga, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwaunganisha wanawake na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Fadhil, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyamihuu, Kata ya Nzihi, Tarafa ya Kalenga, alisema kuwa ameshuhudia kwa karibu namna wanawake wanavyohamasishwa kujitegemea kupitia vikundi vya maendeleo na shughuli za uzalishaji mali, hali iliyomfanya aone umuhimu wa kuchangia katika jitihada hizo.
“Nimeguswa sana na kazi inayofanywa na Diwani wetu wa Kata ya Kalenga katika kuwaunganisha wanawake na kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Nimeona ni jambo la muhimu kutoa mchango wangu ili kuunga mkono jitihada hizi ambazo zina manufaa makubwa kwa jamii nzima,” alisema Fadhil.
Aliongeza kuwa maendeleo ya wanawake ni msingi muhimu wa maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla, hivyo kuna haja ya wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kuweka mazingira yatakayowawezesha wanawake kufikia malengo yao.
Aidha, alisema ataendelea kushirikiana na viongozi na wadau wengine katika kusaidia miradi mbalimbali inayolenga kuinua maisha ya wanawake na vijana wa Tarafa ya Kalenga.
Kwa mujibu wa Fadhil, juhudi za kuwawezesha wanawake zinaendana moja kwa moja na maono na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa kuhimiza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na maendeleo jumuishi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kalenga, Shakira Kiwanga, alimpongeza Fadhil Mgeni kwa mchango wake mkubwa na moyo wa kujitolea katika kusaidia maendeleo ya wanawake wa eneo hilo.
Shakira alisema kuwa mafanikio ya kuanzishwa kwa jukwaa hilo yametokana na ushirikiano wa viongozi, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi waliotoa mchango wao kwa namna mbalimbali.
Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wote waliofanikisha uzinduzi wa jukwaa hilo, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na watu wengine waliochangia kwa hali na mali kufanikisha tukio hilo.
“Tunawashukuru sana wadau wote waliotuunga mkono. Ushirikiano huu unaonesha namna jamii yetu ilivyo tayari kuwawezesha wanawake kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa,” alisema Shakira.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi, alimshukuru Fadhil Mgeni kwa mchango wake huku akieleza kuwa jukwaa hilo litakuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake wa Tarafa ya Kalenga.
Alisema jukwaa hilo litasaidia kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi, kuwapa elimu mbalimbali za maendeleo na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika nafasi za maamuzi na uongozi.
Zainabu alisisitiza kuwa wanawake wakipewa fursa na kuwezeshwa ipasavyo wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya katika familia na jamii kwa ujumla.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Happines Pima ambae ni meneja wa benki ya NMB tawi la Mkwawa alisema wao kama benki wanaunga mkono jitihada hizo.
Uzinduzi wa Jukwaa la Wanawake Kiuchumi, Maendeleo na Siasa la Tarafa ya Kalenga umeonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya eneo hilo, huku wadau mbalimbali wakiahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.












0 Comments