TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII
NA MATUKIO DAIMA.
Serikali wilaya ya Iringa imeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mchango wake mkubwa katika ukusanyaji wa mapato yanayowezesha utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, huku ikisisitiza kuwa mafanikio ya taifa yanategemea uwepo wa mfumo imara wa ukusanyaji wa kodi.
Akizungumza katika hafla ya upandaji miti iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta alisema TRA imeendelea kufanya kazi nzuri kwa miaka 30 tangu kuanzishwa kwake licha ya changamoto zinazokabili jukumu la ukusanyaji wa mapato.
Alimpongeza Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, pamoja na watumishi wote wa mamlaka hiyo kwa uongozi na juhudi zao katika kuongeza makusanyo ya mapato, akibainisha kuwa bila mapato ya serikali huduma muhimu kama afya, elimu, mishahara ya watumishi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo usingewezekana.
“Ninaipongeza TRA kwa kuadhimisha miaka 30 kwa kurejesha fadhila kwa jamii kupitia shughuli mbalimbali zikiwemo upandaji miti, akisema hatua hiyo inaonesha kuwa mamlaka hiyo si mkusanyaji wa kodi pekee bali pia ni mshirika katika uhifadhi wa mazingira”alisema Sitta
Mganga MKuu mfadhidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Alfredy Mwakalebela akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti hospitalini hapo, alisema TRA imekuwa ikiendesha shughuli mbalimbali za kuwathamini wadau wake, na sasa imepanua wigo kwa kushirikiana moja kwa moja na jamii kupitia miradi yenye manufaa kwa wananchi.
“Tunashukuru kwa hatua ya kupanda miti katika eneo la hospitali ni muhimu kwa kuwa itaboresha mazingira ya hospitali kwa manufaa ya wagonjwa,wahudumu wa afya na wananchi wanaopata huduma hususani katika maeneo yanayozunguka jengo la wazazi, na hivyo kuwapatia wagonjwa na wanaofika hospitalini mazingira bora na salama”alisema Mwakalebela.
Aidha, alieleza kuwa baadhi ya miti iliondolewa wakati wa ujenzi wa miundombinu ya hospitali, hivyo msaada wa TRA wa kupanda miti mipya utasaidia kurejesha uoto wa mazingira uliopungua.
“Tunaishukuru TRA kwa msaada wa miche ya miti pamoja na kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika shughuli za maendeleo na uhifadhi wa mazingira”
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa Maigloria Saria alisema zoezi la upandaji miti limefanyika nchi nzima Juni 28 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na maandalizi ya kilele cha utoaji wa Tuzo za walipa Kodi Bora kitakachofanyika Julai 1.
Alisema pamoja na jukumu la ukusanyaji wa kodi, TRA imeamua kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti katika taasisi mbalimbali, ikiwa ni ishara ya dhamira ya mamlaka hiyo ya kuchangia maendeleo endelevu ya jamii.
Alisema kuwa mbali na upandaji miti, maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yanajumuisha shughuli nyingine za kijamii zikiwemo matembezi ya hisani na kampeni za kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari, zikilenga kuimarisha uhusiano kati ya TRA na wananchi.
Naye mmoja wa wafanyakazi wa TRA Ezekiel Makala alisema upandaji miti ni miongoni mwa matukio mbalimbali yaliyoandaliwa kuadhimisha miaka hiyo tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Alisema miti ni muhimu katika kuhifadhi mazingira na maisha ya viumbe hai, hivyo wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kupanda na kuitunza ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha Ezekiel alitoa wito kwa wananchi kudai risiti kila wanaponunua bidhaa au huduma, huku akiwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa risiti kwa wateja wao kwa mujibu wa sheria.
“Ushirikiano huu utasaidia kuongeza mapato ya serikali na kujenga uchumi imara unaojitegemea, ambao utawezesha utoaji wa huduma za kijamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini”alisema





















0 Comments