Header Ads Widget

WANANFUNZI WAHIMIZWA KUWA MSTARI WA MBELE KUTUNZA MAZINGIRA

 


MKURUGENZI wa Idara ya Elimu ya Maandalizi na Msingi, Fatma Ramadhan Mode, amewahimiza wanafunzi kuwa mstari wa mbele katika kutunza mazingira yanayowazunguka, akisisitiza kuwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii yanategemea mazingira salama na endelevu.

Aliyasema hayo wakati akihitimisha mdahalo wa siku tatu wa wanafunzi wa skuli za msingi kuhusu utunzaji wa mazingira, ulioandaliwa na shirika la SOS kupitia Mradi wa Kuimarisha Familia katika maeneo  yanayotekelezwa mradi huo.

Alieleza kuwa watoto ndio walinzi wa kwanza wa mazingira ya kesho, hivyo ni muhimu kuwajengea uelewa huo mapema ili wawe sehemu ya suluhisho la changamoto za kimazingira zinazoikabili dunia hivi sasa

“Tunapowafundisha watoto kuhusu mazingira tunakuwa tunajenga taifa lenye uwajibikaji, lenye afya bora na lenye uwezo wa kulinda rasilimali zake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Fatma.

Alisema mazingira bora huchangia kukuza sekta mbalimbali ikiwemo utalii, kilimo, afya pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla, hivyo kila mwanafunzi anapaswa kuwa balozi wa usafi na uhifadhi wa mazingira katika eneo analoishi.

“Tunapolinda mazingira yetu tunalinda maisha yetu, uchumi wetu na kizazi kijacho. Mazingira safi ni msingi wa maendeleo ya taifa,” alisema Fatma.

Aidha aliipongeza SOS kwa kuandaa mdahalo huo ambao umewapa wanafunzi nafasi ya kujifunza, kujieleza na kuwa na uelewa na uthubutu wa kushiriki kikamilifu katika masuala ya uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mratibu wa Vijana na Jinsia Taifa kutoka Shirika la Kimataifa la Watoto Zanzibar (SOS), Evelyne Baruti, alisema shughuli za kibinadamu zimechangia kuongezeka kwa athari za tabianchi ikiwemo kuathirika kwa ozone layer na kusababisha mifumo ya mvua kutokuwa ya kutabirika.


Alisema hali hiyo imekuwa chanzo cha kupoteza maisha ya watu pamoja na rasilimali muhimu kutokana na mafuriko, ukame na majanga mengine yanayotokana na uharibifu wa mazingira.

“Tunapaswa kutunza mazingira leo ili nayo yatutunze kesho. Bado tunakabiliwa na janga la utupaji wa taka za plastiki ambalo linahitaji elimu na hatua za pamoja,” alisema Evelyne.

Aliongeza kuwa lengo la mdahalo huo ni kukuza vipaji vya watoto katika kuzungumza na kujenga hoja mbele za watu, kuongeza uwezo wao wa kujieleza, kuwajengea uelewa sahihi wa masuala ya mazingira pamoja na kuwaandaa kuwa mabalozi wa mazingira kwa wenzao.

"SOS ina mpango wa kuwakuza vijana hao kuwa mabalozi wazuri wa mazingira na niwaombe walimu kusimamia klabu za mazingira maskulini ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kuendeleza ujuzi walioupata." Alisema 

Baadhi ya wanafunzi washiriki  walitetea hoja mbalimbali ikiwemo 'Sheria kali za mazingira zinafaa zaidi kuliko elimu ya mazingira' wakisema sheria huleta matokeo ya haraka kuliko elimu, kwani huwafanya watu kufuata utaratibu bila kujali kama wameelimishwa au la.

Mwanafunzi Hajra Ali Suleiman kutoka Skuli ya msingi  Bububu A alisema sheria humzuia mtu kufanya vitendo visivyoruhusiwa na hurahisisha kuwachukulia hatua waharibifu wa mazingira.

“Elimu bila sheria ni sawa na gari bila breki. Sheria huweka nidhamu na kuzuia uharibifu kwa kiwango kikubwa,” alisema Hajra.

Naye mwanafunzi Intsaar Suleiman Khamis alisema hata kama watu wataelimishwa bila kuwepo sheria na adhabu, bado baadhi yao wataendelea  kuharibu mazingira Kwa njia mbalimbali.

Kongamano hilo lilihusisha skuli nane za msingi ambapo kila skuli iliwakilishwa na wanafunzi 10 pamoja na walimu wawili, huku mada mbalimbali zikiwasilishwa ikiwemo umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na changamoto za uharibifu wa mazingira ambapo Katika fainali ya mdahalo huo, Skuli ya kijichi iliibuka ushindi baada ya kuchuana na Skuli  ya Bububu A kupitia mada iliyosema “Sheria kali za mazingira zinafaa zaidi kuliko elimu ya mazingira.”

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI