Header Ads Widget

WATENDAJI WAAPISHWA ,SERIKALI YAKAZA KAMBA KULINDA RUZUKU YA KOROSHO

 

Na Matukio Daima Media Ulanga

HATUA ya Serikali kuwaapisha watendaji wanaosimamia ugawaji wa pembejeo za ruzuku ya korosho imeelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuzuia wizi, ubadhirifu na vitendo vya rushwa, huku ikisisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuhujumu mpango huo atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.


Kabla ya kuanza rasmi kwa ugawaji wa pembejeo za ruzuku katika Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro, maafisa kilimo pamoja na watendaji wa vijiji wanaapishwa mbele ya mwanasheria na kuahidi kusimamia zoezi hilo kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia sheria na miongozo ya Serikali.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Simba, amesema Serikali imeamua kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha pembejeo zinazotolewa kupitia ruzuku zinawafikia wakulima waliokusudiwa na hakuna nafasi ya hujuma katika mchakato mzima wa ugawaji.


Amesema mtumishi yeyote atakayebainika kuhusika na upotevu wa pembejeo, ubadhirifu, rushwa au kuwanyima wakulima haki zao, atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali nafasi yake.


Pia akawataka wakulima kuwa sehemu ya usimamizi wa zoezi hilo kwa kutoa taarifa wanapobaini ukiukwaji wowote, akieleza kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.


Kaimu Meneja wa Tawi la Bodi ya Korosho Tanzania Mkoa wa Morogoro, Japhari Matata, amesema bodi hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha pembejeo za ruzuku zinawafikia wakulima kwa wakati ili kuongeza uzalishaji na ubora wa korosho.

Amesema mafanikio ya mpango huo yanategemea uwajibikaji wa watendaji pamoja na matumizi sahihi ya pembejeo na wakulima wenyewe.

Afisa Kilimo wa Kata ya Lukande, Alfred Kilasi, amesema sambamba na ugawaji wa pembejeo, maafisa ugani wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo ili kuongeza tija ya uzalishaji.

Kwa upande wao, wakulima wa Wilaya ya Ulanga wameeleza kuwa ruzuku ya pembejeo imekuwa nafuu kubwa kwao, lakini wanaiomba Serikali kuendelea kuboresha huduma za ugani, kuongeza upatikanaji wa mitaji nafuu na kuhakikisha pembejeo zinawafikia kwa wakati kila msimu.

Wamesema endapo usimamizi wa ugawaji utaendelea kuwa wa haki na uwazi, mpango huo utaongeza uzalishaji wa korosho, kuboresha kipato cha wakulima na kuimarisha mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI