Header Ads Widget

RC MAKAME AKUMBANA NA KILIO CHA UKOSEFU MAJI NA KUBAMBIKIWA BILI ILEJE.

 


Na Moses Ng’wat, Ileje.

WANANCHI wa kijiji cha Ikumbilo, kata ya Chitete, wilayani Ileje mkoani Songwe, wamelalamikia tatizo la ukosefu wa maji, licha ya kuwepo kwa miundombinu ya huduma hiyo katika kijiji chao.

Mbali na kukosa maji, wananchi hao wamedai kuendelea kutozwa bili za kila mwezi huku wakieleza kuwa huduma ya maji haipatikani kwenye mabomba yao kwa uhakika.

Kero hiyo iliibuliwa Mei 6, 2026 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, alipofanya ziara ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika kijiji hicho



Akizungumza kwa hisia, mkazi wa Ikumbilo, Mariam Mtafya, alisema haieleweki ni kwa nini wanaendelea kutozwa malipo ya maji kila mwezi wakati hawapati huduma hiyo ipasavyo.

“Hatuelewi kwanini bili za maji zipo pale pale wakati hatujachota maji; unakuta maji yanatoka mara mbili tu kwa mwezi,” alisema Mtafya.

Kwa upande wake, mkazi mwingine, Rehema Mwampashe, alisema upatikanaji wa maji ni wa nadra sana, wakati mwingine hutoka mara mbili kwa mwezi, lakini bado wanalazimika kulipa kiasi kinachofanana cha shilingi 5,000 kila mwezi.



Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ileje, Felister Benson, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa inachangiwa na matumizi yasiyo na nidhamu miongoni mwa watumiaji.

Alifafanua kuwa tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 lililopo kijijini hapo linapaswa kudumu kwa siku mbili, lakini mara nyingi maji hayo huisha ndani ya saa tatu baada ya kujazwa.

Benson aliongeza kuwa tatizo jingine ni ukosefu wa mita za maji, hali inayochochea matumizi holela, huku akibainisha kuwa RUWASA imeanza kuwafungia mita wananchi, ambapo hadi sasa jumla ya wateja 58 wamefungiwa.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa Makame aliagiza kuhakikisha wateja wote wanafungiwa mita ili kila mmoja alipe kulingana na matumizi yake halisi ya maji.


Aidha, alimwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, kusimamia kwa karibu suala hilo ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayedaiwa bili bila kupata huduma ya maji.

Makame pia aliwataka maofisa wa RUWASA kuongeza uwajibikaji na kuwa wepesi kushughulikia hitilafu zinazojitokeza katika miundombinu ya maji.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Songwe kusogeza huduma karibu na wananchi na kutatua changamoto zao katika ngazi za chini bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta msaada.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI