Header Ads Widget

WANANCHI BUKOBA WATAKA KUFUNGULIWA KWA KITUO KIDOGO CHA MAGARI

 

Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera

Wananchi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameuomba uongozi wa manispaa hiyo kufungua kituo kidogo cha mabasi kilichopo katikati ya mji, wakieleza kuwa hatua hiyo itapunguza adha wanayokumbana nayo abiria wanaosafiri kutoka Bukoba mjini kwenda wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wananchi akiwemo Abdrazak Michael amesema kuwa uwepo wa kituo kidogo cha mabasi inasaidia kukuza uchumi wa watu wengi kutokana na kuhusisha wananchi wengi katika eneo hilo.

“kitendo cha kubomoa hii stendi na magari kuyahamishia sehemu nyingine kama Kagondo watu wametawanyika, kama stendi imekamilika zaidi ya asilimia tisini basi tunaiomba serikali stendi hii ifunguliwe ili watu warudi katika sehemu hii waweze kufanya biashara”

Aidha naye Abdul Bamanyisa ameeleza kuwa mara baada ya kufungwa kwa kituo hicho kidogo cha mabasi mzunguko wa kifedha katika mji huo umekuwa mdogo hali inayopelekea ugumu wa maisha na kutaka kama kituo hicho kimekamilika kwa kiasi kikubwa basi kifunguliwe.

“mzunguko wa fedha umekuwa mdogo tangu ifunge stendi hii tunaomba ifunguliwe kama imekamilika ili kuruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea na kukuza mzunguko wa kifedha”

Akizungumza katika baraza la madiwani Diwani wa kata ya Bilele Tawfiq Sharifu amesema kuwa kituo hicho ni hitaji muhimu kwa wananchi wa mji wa Bukoba na kutaka kutolewa kwa taarifa sahihi ya ni lini kituo hicho kufunguliwa kutokana na kutangazwa mara kadhaa kufunguliwa kwa kituo hicho lakini hakifunguliwi.

“mahitaji ya stendi ile mheshimiwa mstahiki meya ni makubwa na muda umekuwa mrefu, tunaomba mkurugenzi atuambie ni siku gani na tarehe ipi stendi hii inafunguliwa tumekuwa tukiambiwa mwezi wa kumi na moja mara mwezi wa tatu leo tuko mwezi wa tano, mara inafunguliwa muda sio mrefu”

Akitolea majibu suala hilo mkurugenzi mtendaji wa manispaa ya Bukoba Jacob Nkwera amesema kuwa kituo hicho cha mabasi kimekamilika kwa kiasi kikubwa ila kinachokwamisha kufunguliwa kwa kituo hicho ni kutokamilika kwa barabara ya kuingia na kutoka katika kituo hicho.

“mheshimiwa mstahiki meya kinachokwamisha kutofunguliwa kwa stendi hiyo ni kutokana na njia ya kuingia kwenye stendi hiyo ila tunatafuta namna ya kukamilisha barabara hiyo na muda sio mrefu itafunguliwa baada ya barabara kukamilika”

Ujenzi wa kituo kidogo cha mabasi katika mji wa Bukoba uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa sasa umefikia asilimia 99 ya ujenzi wake kwa awamu ya tatu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI