Na Josea Sinkala, Chunya Mbeya.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Tamim Kambona, amewataka watoa huduma wa Afya katika Hospitali ya wilaya ya Chunya kuendelea kutoa huduma bora ili Hospitali hiyo iwe nafasi ya kwanza nchi katika utoaji wa huduma.
Ametoa kauli hiyo Mei 06, 2026 ofisini kwake wakati akikabidhiwa cheti ikiwa ni zawadi ambayo Halmashauri ya Chunya imeipata (Hosptiali ya wilaya ya Chunya) baada ya kushika nafasi ya pili kitaifa katika utoaji wa huduma wakati wa kilele cha siku ya Afya iliyofanyika Mkoani Pwani.
“Mwaka jana tulikuwa nafasi ya tatu na unaweza kukuta wale tulioshindana nao mwaka jana wote hawajafanya vizuri lakini sisi Chunya kwa mara nyingine tumejitokeza katika nafasi na tumepata nafasi ya juu ambayo ni nafasi ya pili, naomba sasa ongezeni kasi ya kuwahudumia wananchi ili hatimaye mashindano haya yatakapokuja mwaka mwingine tuwe nafasi ya kwanza” amesema Kambona.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Chunya Dkt John Gungumka, amesema wataendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi wa Chunya ili kufikia azma njema ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi wao.
Aidha Dkt. Gungumka amemshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya pamoja na viongozi wengine kwa namna wanavyoendelea kuwapa ushirikiano watoa huduma wa Afya katika Hospitali ya wilaya ya Chunya huku akiendelea kuomba ushirikiano huo zaidi ili kuendelea kuleta ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi wa Chunya na watanzania wengine kwa ujumla hasa waishio wilayani Chunya.
Hospitali ya wilaya ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya imeng’ara katika mashindano ya afya kitaifa kwa kunyakua nafasi ya pili katika ya Hospitali za wilaya mia moja sitini na saba (167) zilizoshindanishwa, ambapo kilele cha mashindano hayo kilifanyika Aprili 29, 2026 katika Halmashauri ya Kibiti mkoani Pwani.


.jpeg)




0 Comments