Na Lilian Kasenene, Morogoro-Matukio DaimaApp
JESHI la Magereza limeitaka jamii kuacha unyanyapaa kwa wafungwa wanaomaliza vifungo vyao na kurudi uraiani ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na uzalishaji.
Kamishna wa Huduma za Urekebu wa Jeshi hilo, Amina Semina Kavirondo, amesema wafungwa wanaomaliza vifungo vyao hurudi uraiani wakiwa na ujuzi mbalimbali, lakini hushindwa kuutumia kutokana na jamii kutowaamini.
“Wafungwa wakati wa kutumikia vifungo vyao wanaandaliwa vizuri na wanapotoka wanakuwa na ujuzi. Changamoto kubwa wanayokutana nayo wakirudi uraiani ni unyanyapaa,” alisema Kamishna Kavirondo.
Alisema jamii kwa kushirikiana na serikali inapaswa kuwaamini na kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji ili kuepuka kurudi kwenye vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuwarudisha magerezani.
Kamishna Kavirondo aliyasema hayo wakati wa mafunzo ya uzalishaji wa nishati safi kwa askari magereza kutoka nchini kote yanayofanyika katika Gereza la Kihonda, mkoani Morogoro.
Alieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo askari hao ili waweze kwenda kutoa ujuzi huo kwa wafungwa waliopo magerezani, na hivyo kuwasaidia kutumia maarifa hayo baada ya kumaliza adhabu zao.
Akifungua mafunzo hayo, Kamishna wa Mipango na Fedha wa Jeshi la Magereza, Chacha Bina, alisema tayari mashine 61 za kutengeneza mkaa safi zimefungwa katika vituo mbalimbali nchini.
Kamishna Bina alisema mashine hizo zinazozalisha mkaa mbadala kwa kutumia mabaki ya mimea zitasaidia pia katika utunzaji wa mazingira.
“Uzalishaji wa mkaa kwa kutumia mashine hizi, ambazo malighafi yake ni mabaki ya mimea, utasaidia kupunguza gharama, kutunza mazingira na kuongeza kipato kwa Jeshi la Magereza,” alisema Kamishna Bina.
Aliongeza kuwa askari wanaopata mafunzo hayo watakwenda kuyatekeleza kwa vitendo kwa kuwafundisha wafungwa, ili wanapomaliza adhabu na kurudi uraiani wawe na ujuzi wa kujitegemea badala ya kurejea kwenye uhalifu.
Naye Mkuu wa Gereza la Kihonda, Lucas Mboje, alisema pamoja na kutoa ujuzi kwa wafungwa, mkaa huo pia utauzwa kwa wananchi ili kuongeza mapato ya jeshi hilo.
“Mabaki ya mimea yalikuwa yakionekana kama uchafu, lakini sasa yatakuwa biashara kwani ndiyo malighafi ya uzalishaji wa mkaa safi. Lengo letu ni kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mkaa kwa kipindi chote,” alisema Mboje.








0 Comments